NA MWANDISHI WETU
WAKONGWE wa soka nchini, Zamoyoni Mogella na Ally Mayay, Mwisho mwa wiki walizindua rasmi duka la kimataifa la vifaa vya michezo la liitwalo Anta ambalo lipo chini ya Kampuni ya GSM Group.
Duka hilo litakalouza vifaa vya michezo kama jezi, viatu, soksi na vinginevyo, litapatikana Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi huo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa GSM Group, Matina Nkurlu, alisema duka hilo litatambulika kwa jina la Anta Store, likiwa na bidhaa zenye ubora wa kiwango cha kimataifa zitakazopatikana kwa bei nafuu.
“GSM Group tunayo furaha kubwa kuwatangazia habari njema wanamichezo na wapenzi wa michezo kuwa tumewaletea duka la vifaa vya michezo vyenye ubora wa kimataifa kwa bei nafuu kabisa, hivyo wadau mbalimbali wa michezo wajitokeze katika duka hilo lililopo Mlimani City ili kujipatia bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kulingana na mahitaji na uwezo wao,” alisema.
ANTA ni brand ya kimataifa inayotengeneza na kuuza vifaa vya michezo. Kampuni ilianza mwaka 1994, nchini China na kupata umashuuri kwa haraka sana duniani kote. GSM imeingia mkataba na wazalishaji hawa kuwa ndio wakala pekee mkubwa ya chapa ANTA hapa Tanzania.
Huko Ulimwenguni, ANTA imeingia mkataba na wanamichezo wakubwa kama bondia Manny Pacquiao pamoja na mchezaji wa mabingwa wa NBA Basketball ya Golden State Warriors aitway Klay Thompson pamoja na wanamichezo mingi
Alisema kwamba wameamua kuwahusisha Mogella na Mayay katika uzinduzi huo kama sehemu ya kuthamini mchango wao katika medani ya michezo hapa nchini, hususan soka, unaoongoza kwa kupendwa duniani kote.
“Licha ya kuwa wamekuja wanamichezo hawa wachache, ANTA itakua inauza bidhaa kwa karibu fani zote za michezo duniani”.
Kwa upande wake, Mogella aliyewahi kuwa mfungaji hatari wa Simba, Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars, aliipongeza GSM kwa kufungua duka hilo na kuwataka wapenzi wa soka hapa nchini kujitokeza kwa wingi katika duka hilo ili kujipatia vifaa vya michezo vyenye ubora.
Naye Mayay, alisema: “Vifaa vya michezo vinavyopatikana katika dula la Anta lililopo chini ya GSM pale Mlimani City, ni vya viwango vya kimataifa hivyo Watanzania wasisite kufika pale Mlimani City kujipatia bidhaa bora kabisa tena kwa bei nafuu.”
Mbali na wanasoka hawa, pia uzinduzi huu ulishuhudiwa na wadau wengine katika michezo wakiwemo wanariadha na Bondi mashuhuri nchini Mfaume Mfaume.
Mbali ya duka hilo, GSM Group wana maduka mengine ya bidhaa mbalimbali kama mavazi, vyombo vya nyumbani, fenicha, vifaa vya umeme na vinginevyo yanayopatikana Mlimani City Mall, Pugu Mall na kwingineko.