Miamba ya soka ya Premier League, Manchester United imeendelea kuwa kileleni kwenye maswala uingizaji wa mapato ngazi ya klabu England.
United imezidi kuwa moto wa kuotea mbali mbele ya miamba mengine ya soka pale Premier League zikiwemo Manchester City na Liverpool ambazo zikiwa nyuma ya mashetani hao wekundu.
United imeingiza kiasi cha pauni milioni 627.1 msimu wa mwaka 2018/19 na kuwafanya kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa klabu nyuma ya wafalme wa soka wa Hispania Barcelona wenye pauni milioni 741.1 wakiwa nafasi ya kwanza na Real Madrid pauni milioni 667.5 wakiwa wa pili katika jarida hilo.
Giants’ wengine wa Premier League wakiwa karibu kabisa na United ni Man City ambao wana pauni milioni 538 wakiwa nafasi ya sita huku Liverpool iliyopo nafasi ya saba ikijikusanyia pauni milioni 533, wakati Tottenham Hotspur ikiwa nafasi ya nane kwa kuingiza kitita cha pauni milioni 459.3 huku Chelsea wakiwa wa tisa kwa kuingiza pauni milioni 452.2.
Manchester United imeonekana kuwa vizuri katika mapato licha ya klabu hiyo kushindwa kutwaa taji la ligi kwa muda sasa.
United imekuwa kwenye kiwango cha hali ya juu katika mkwanja ndani ya English tangu kuanzishwa kwa mfumo wa kuangazia uingizaji wa mapato kwa klabu ‘Deloitte’s Football Money League’