Home Uncategorized BOCCO ASHINDWA KUJIZUIA, AAMUA KULIIBUA TENA SUALA LA MAPINDUZI

BOCCO ASHINDWA KUJIZUIA, AAMUA KULIIBUA TENA SUALA LA MAPINDUZI


Nahodha na mshambuliaji wa Simba, John Raphael Bocco amesema kuwa haikuwa bahati yao kulichukua Kombe la Mapinduzi huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwaunga mkono watakaporejea kwenye Ligi Kuu Bara.

Simba wiki jana ilikosa kombe hilo kwa kufungwa katika hatua ya fainali ya michuano hiyo iliyomalizika kwa Mtibwa Sugar kuchukua taji hilo kwa ushindi wa bao 1-0, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja, Zanzibar.

Mtibwa walipata ushindi huo kupitia kwa Awadh Salum aliyefunga bao dakika ya 39 ya mchezo huo baada ya kuupokea mpira uliopigwa na Jaffary Kibaya.

Bocco alisema kuwa katika mchezo huo walitengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao lakini walishindwa kuzitumia kutokana na kukosa umakini wakiwa ndani na nje ya 18.

Bocco alisema kuwa hivi sasa nguvu na akili zao wamezielekeza katika ligi baada ya kulikosa kombe hilo.

“Haikuwa bahati yetu, nawapongeza Mtibwa kwa kucheza vizuri na kufanikiwa kuchukua kombe walilokuwa wanaliwania mwaka huu baada ya kulikosa kwa miaka kadhaa.

“Baada ya kulikosa kombe hilo, niwaombe mashabiki wa Simba kuendelea kuisapoti timu kwenye Ligi Kuu Bara, kwa kuwa matokeo haya ni sehemu ya mchezo wa soka na wala wasiwe na presha.

“Kocha ameona makosa yetu, hivyo ninaamini kuwa atayafanyia kazi makosa yetu ili tutakaporejea katika ligi tuendelee na kasi yetu ya ushindi kuhakikisha tunaendelea kukaa kileleni hayo ndiyo malengo yetu, mashabiki watupe sapoti katika hili tutapambana kupata matokeo” alisema Bocco.
SOMA NA HII  WAWA ACHEKELEA MAISHA YAKE NDANI YA SIMBA