Nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul, amesema kuwa uwezo alionao kiungo mshambuliaji, Bernard Morrison, raia wa Ghana, ni habari nyingine kwani ana vitu vingi vya kipekee akiwa uwanjani.
Yanga imecheza mechi 15 za ligi, ipo kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara ulio mikononi mwa Simba ambao ni watani zao wa jadi, ipo nafasi ya nne kwenye ligi ikiwa na pointi 28, tofauti ya pointi 13 za Simba iliyo na pointi 41 ikiwa imecheza mechi 16.
Abdul alisema kuwa kwa muda ambao wamekuwa na nyota huyo, wamegundua vitu vingi anavyo jambo linalowapa matumaini ya kufanya vizuri.
“Morisson ni mchezaji mzuri na ana maelewano na wachezaji wengine wote wa Yanga, kwa namna anavyokuja vizuri, tuna imani ya kuendelea kuwapa burudani mashabiki na kufanya vema kwenye mechi zetu za ligi.
“Hana tabia ya uchoyo wa pasi na akiwa na kitu anawashirikisha wengine, unajua tunaishi maisha ya kushirikiana, kikubwa tunamuomba Mungu tufikie malengo yetu, mashabiki watupe sapoti,” alisema Abdul.