KIPA namba moja wa Yanga, Farouk Shikalo Jumatano ya wiki hii aliondoka nchini na kurejea kwao Kenya kwa ajili ya kwenda kutatua matatizo ya kifamilia.
Imeelezwa kuwa staa huyo amekwenda kumuuguza mmoja wa watu wa familia yake ambapo atarejea nchini leo Ijumaa.
Shikalo ambaye alisajiliwa na Yanga akitokea Bandari aliondoka nchini juzi na kukosa mazoezi ya kikosi hicho yaliyofanyika katika Chuo cha Sheria, Ubungo ambapo kwenye mazoezi hayo alikuwepo kipa mmoja tu Metacha Mnata.
Kocha wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael amelieleza Championi Ijumaa, kuwa kipa huyo aliondoka nchini na kurejea kwao Kenya baada ya kuomba ruhusa ya siku tatu kwa ajili ya kwenda kumuuguza mmoja ya watu wa familia yake.
“Shikalo aliomba kuondoka na kwenda kwao kwa ajili ya kumuuguza mmoja ya watu wa familia yake. Lakini ruhusa hiyo ni ya siku tatu na baada ya hapo atarudi tena kwa ajili ya kujiunga na timu kama ilivyo kwa wenzake,” alisema Mbelgiji huyo.