Home Uncategorized TUSIIUE HOJA YA MSINGI KWA KISINGIZIO SIMBA INAPENDELWA…

TUSIIUE HOJA YA MSINGI KWA KISINGIZIO SIMBA INAPENDELWA…


NA SALEH ALLY
NATAKA niende moja kwa moja kuwa nimekuwa nikikerwa na propaganda zinazoenezwa na baadhi ya watu ambao ninaamini wameshindwa mambo.


Mjadala huu unachombezwa na baadhi ya mashabiki ambao wanaonekana wameshindwa kujitambua, wameshindwa kuelewa kuwa wanatumika vibaya na baadhi ya viongozi ambao wameshindwa majukumu yao.


Kuna propaganda ambayo haina faida na afya ya mchezo wa soka nchini kuendelea kulazimisha ionekane waamuzi wanaipendelea sana Simba.


Katika hali ya kawaida, mimi kama mdau wa mpira siwezi kuungana mkono hata kidogo na waamuzi ambao ningeona wana nia hiyo.


Kama wangekuwa kweli wanaipendelea Simba, bila shaka tungepiga kelele na kukemea kwa kuwa kukua kwa mpira wa Tanzania, suala la haki linatakiwa kuchukua nafasi kubwa sana.

Binafsi ninapinga kama kweli kuna waamuzi wana mawazo au nia ya kutaka kuipendelea timu fulani ambalo si jambo sahihi na halina msaada hata kidogo kwa maisha ya ukuaji wa mpira wa Tanzania.


Pamoja na hivyo, nataka kuwaasa wale ambao wamekuwa bendera fuata upepo, wanalibeba suala hili bila ya kuliangalia kwa kina.


Simba ambayo sasa imefunga mabao 40 katika mechi 17, imependelewa mangapi ambayo wanaweza wakayaelezea na kuwaaminisha watu.


Tumeona waamuzi hawa wanakosea katika mechi hata zinazoihusisha Yanga na timu nyingine na si Simba tu, tumeona wanakosea hata katika mechi za Azam FC au za timu nyingine na wachezaji au viongozi wa timu za Ligi Kuu Bara wanalijua hili.


Simba imefunga mabao 40, ukiangalia  Yanga wamefunga 20, baada ya bao la jana dhidi ya Mtibwa Sugar, Lipuli wana mabao 23, Azam FC yenye 22. Tuambiwe kwa takwimu Simba kapendelewa mara ngapi badala ya hadithi tu.


Kwangu suala la Simba kapendelewa kama hakuna takwimu basi inakuwa ni kubabaisha tu mambo na kutaka kuhamisha hoja ya msingi ambayo tunapaswa kuizungumza.


Mimi nimesema waamuzi wanakosea katika mechi nyingi hata zile ambazo haziihusishi Simba na tunaona. 


Maana yake hapa, hoja ya msingi ni suala la waamuzi kuwa na kiwango duni katika utekelezaji wa kazi zao na hapa ndipo tunapaswa kupashikilia kwa ajili ya mpira wa Tanzania.


Tupunguze ushabiki katika mambo ya msingi, kila mara nimekuwa nikisema hakuna timu inayomiliki waamuzi na wanapokuwa wanavurunda, sote tunafahamu wapi pa kwenda na kuwakumbusha kuwa mambo yanaharibika.


Kuendelea kulia Simba inapendelewa wakati waamuzi wanakosea, ni kufunika makosa yao kupitia ushabiki, huenda kutengeneza hisia za wengine pia kupendelewa ili tuwe na ligi ya wanaopendelewa tu, jambo litatufanya tuwe na akili za hovyo kabisa.


Waamuzi wanavurunda na hili ndilo suala linatakiwa kufanyiwa kazi, wapate maonyo au kuchukuliwa hatua kali kwa wale wote wanaoboronga.


Unaona mechi ya watani Yanga na Simba, bila ya ubishi, ilionekana penalti waliyopewa Simba ina utata na kweli haikuwa penalti na hili ni kosa la ‘assistant line two’. Bao la pili la Yanga nalo lilikuwa na makosa sahihi kusema si bao kwa kuwa Mohamed Issa Banka alimsukuma kabisa Mohamed Hussein Zimbwe aliyejifunga lakini ‘assistant line two’ huyohuyo akajikausha ili kufunika kosa la kwanza kwa ‘kubalansi’.


Hii maana yake, hawa waamuzi wanajua matatizo yao na wanachokosea. Hivyo tusiwape nafasi kabisa ya kuendelea kurekebisha makosa yao kupitia makosa, wataziumiza timu.


Maana timu moja itaumizwa kwa makosa na udhaifu wa ubora wa mwamuzi halafu yeye atajirekebisha kwa kuiumiza nyingine tena, hii si sahihi.


Kwa sasa si nani anapendelewa kwa kuwa tukiangalia hivyo, hata wale wanaolalamika wanaweza kukuta timu yao imependelewa zaidi kwa udhaifu wa waamuzi au makusudi.


Hivyo vizuri kudhibiti pale yanapoanza kutokea maji kuliko kusubiri yatoke halafu tuanze kuchota kuyapunguza.


SOURCE: CHAMPIONI

SOMA NA HII  UKIMFUATILIA MO DEWJI UPANDE HUU, UTAGUNDUA JAMBO TOFAUTI