Katika kuisuka safu yake ya ushambuliaji, Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael ametengeneza kombinesheni tatu hatari za kufunga mabao huku akimtumia kiungo wake mshambuliaji mwenye jina kubwa hivi sasa, Mapinduzi Balama ‘Kipenseli’ kucheza namba 10.
Mbelgiji huyo katika mazoezi ya hivi karibuni yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Ubungo jijini Dar es Salaam wakijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Lipuli FC ya mkoani Iringa uliopigwa jana Jumatano, alionekana akitengeneza kombinesheni tatu za ushambuliaji.
Ya kwanza ilikuwa ni Mkongomani David Molinga ‘Falcao’ mwenye mabao sita hivi sasa katika ligi aliyekuwa akicheza namba 9 huku Balama akicheza 10, Bernard Morrison na Deus Kaseke wakitokea pembeni katika kupeleka mashambulizi.
Nyingine ilikuwa na mshambuliaji mwenye umbile kubwa raia wa Ivory Coast, Yikpe Gnamien aliyekuwa akicheza namba 9 na Balama kama kawaida alimtupia 10 kama kiungo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi ambaye yeye kazi yake ni kupokea mipira kutoka kwa Mnyarwanda, Haruna Niyonzima katika kupeleka mashambulizi.
Baada ya hizo mbili, hii ya tatu ndiyo balaa iliyoongozwa na mshambuliaji mwenye kasi na nguvu za kupambana na mabeki wabishi ambaye ni Ditram Nchimbi aliyepewa jina la Duma huku namba 10 kama kawaida akianza na Balama aliyeingia katika kombinesheni zote za washambuliaji wa timu hiyo akisaidiana na Niyonzima ambao wao kazi yao ni kupiga pasi za mabao pekee.
Akizungumzia hilo, Luc alisema kuwa: “Bado timu yangu inapata ushindi mdogo wa mabao, ninataka kuona timu inapata ushindi wa mabao mengi zaidi ya matatu na siyo wa 1-0.
“Ninaendelea kutengeneza timu kwa maana ya kombisheni mbalimbali kwa kuanzia nimeanza na hii ya ushambuliaji ambayo mara nyingi imekuwa ikishindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga ambazo wamekuwa wakizipata.
“Hivyo hivi sasa ninatengeneza kombinesheni za ushambuliaji mazoezini kwa kuwajaribu baadhi ya wachezaji na lengo ni kuona timu ikipata ushindi wa mabao mengi.”