Home Uncategorized KUSHINDA KWA MBINDE KWA SIMBA SI UDHAIFU WA SVEN

KUSHINDA KWA MBINDE KWA SIMBA SI UDHAIFU WA SVEN



Na Saleh Ally
KOCHA Mkuu wa Simba, Sven van der Broeck ndio amefikisha mechi 15 tangu aanze kuinoa Simba akichukua nafasi ya Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji kama ilivyokuwa kwake.


Sven ameiongoza Simba katika mechi hizo 15 katika michuano mitatu tofauti, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Kombe la Mapinduzi ambayo hufanyika visiwani Zanzibar.


Ana mechi 10 za Ligi Kuu Bara, mechi tatu za Mapinduzi Cup na mbili za Kombe la Shirikisho ambalo bingwa wake huiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Caf.


Katika mechi zake mbili za Kombe la Shirikisho, Simba imeshinda zote, ikiitwanga Arusha FC kwa mabao 6-0 pia Mwadui FC kwa mabao 2-1. Kumbuka Mwadui FC ndio ilishinda dhidi ya Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara, kikosi kikiwa chini ya Aussems na ukawa mchezo wa kwanza wa Simba kupoteza msimu huu.


Upande wa michuano ya Mapinduzi ambayo huwa ni pasha mwili maalum kwa ajili ya sherehe za Mapinduzi, Simba ilishinda mbili za kwanza ikiichapa Zimamoto kwa mabao 3-1, ikaishinda Azam FC kwa mikwaju ya penalti 3-2 na kutinga fainali ambalo ililala kwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.


Michuano ya tatu ni Ligi Kuu Bara, hii ndio kipimo namba moja cha Simba na imecheza mechi 10. Kati ya hizo, imeshinda nane, sare moja ya 2-2 dhidi ya Yanga na imepoteza moja ikitolewa jasho na JKT Tanzania kwa kuchapwa kwa bao 1-0, hii juzi.


Hii ndio rekodi kamili ya jumla wa mechi za michuano yote, zipo 15, kati ya hizo, Simba imeshinda 12, sare moja na poteza mbili. Hapa ndipo mjadala unaanzia kwa mashabiki wa Simba, wanaona kocha huyu anapaswa kuondoka, kwa kuwa rekodi yao si nzuri, au aondoke kwa kuwa wana mapenzi sana na Aussems ambaye wakati anaondoka hakuna aliyemzuia abaki, na wengi wakasema aende, au kipi hasa?


Katika mechi za Ligi Kuu Bara, mechi 10, sare moja, kupoteza moja na kushinda 8, inaweza kuwa rekodi inayomfukuzisha kocha?


Kuna neno mashabiki wanalitumia, kuwa wanashinda kwa mbinde, au wanatanguliwa. Je, kinaweza kuwa kigezo cha kumuondoa kocha katika kikosi?


Angalia msimamo wa Ligi Kuu Bara, hadi sasa Simba ndio timu bora. Kwani baada ya mechi 20, imeshinda 16, sare mbili na kupoteza mbili. Inaongoza kwa tofauti ya pointi 9 dhidi ya Azam FC. Yanga ina michezo miwili mkononi, ikishinda yote, tofauti itakuwa pointi 7 lakini kwa sasa ni pointi 13.


Simba ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi ikiwa na 42, mara tatu na nusu zaidi ya Singida United, mara nne zaidi ya Ndanda FC, mara mbili zaidi ya Mtibwa Sugar pia karibu mara mbili ya Yanga ambayo sasa ina mabao 23.


Kwenye kuruhusu mabao, Simba imefungwa 11 ambayo inaifanya kuwa na safu ngumu zaidi ya ulinzi, Singida United ni dhaifu zaidi ikiwa imefungwa 30, inayofuatiwa kwa bora ni Azam FC imefungwa 12 halafu Coastal Union iliyofungwa 14 na Yanga 16.


Sasa mbinde wanaoizungumzia mashabiki wa Simba ni ipi, hawataki timu yao ishindane na vipi wanataka ushindi wa mchekea, wanataka ushindi mlaini huku wakijua Simba inacheza ligi na kama wanashinda kwa kupambana maana yake wana kikosi bora.


Sven anaweza kuwa na upungufu katika kikosi chake, basi anatakiwa kukifanyia kazi na hii ndio kazi ya ukocha. Pia wachezaji, waelezwe nao wajitume na kwa pamoja, wapambane kubadilisha mambo, kuyafanya yawe bora kwa kuongeza umakini na ubora pia kupunguza makosa kwa kiasi kikubwa zaidi. Hivyo acha iwe mbinde lakini wapambane na marekebisho yafanyike.


Haijawahi kuwa duniani, kila timu ikipoteza mechi moja, kocha anafukuzwa. Presha ya mashabiki ndio iliyomuondoa Uchebe, leo wanamlilia. Kesho atakuja kocha mwingine, sababu ya ugeni naye anaweza kupoteza, halafu aondoke. Simba itajichanganya na mfumo wake utakuwa usioeleweka.


Angalia Yanga, baada ya miezi mitatu kufundishwa na makocha watatu tofauti, yaani Mwinyi Zahera, Charles Boniface Mkwasa na Luc Eymael, sasa ndio wanaanza kutulia. Simba wasipoangalia, kwa kufuata mkumbo watajiingiza huku na mwisho watashangaa wanatumbukia ambako hawakutarajia.


Viongozi wawe makini na kelele za mashabiki hata kama ni wenye timu, mambo mengine yanahitaji utaalamu na si hisia au mihemko ya watu.


Kikubwa mashabiki wakumbuke, ubora wa Simba unawafanya wapaniwe na kila mtu, hivyo hakuna mechi watakayocheza ikawa nyepesi. Suala la kiwango kuwa duni, benchi la ufundi lipewe nafasi, liifanyie kazi hilo jambo, haliwezi kuwashinda kwa kuwa watashirikiana na wachezaji.


TAKWIMU:
REKODI YA SIMBA CHINI YA SVEN:

Kombe la FA
Simba 6-0 Arusha 

Ligi Kuu Bara
Simba 4-0 Lipuli
KMC 0-2 Simba
Simba 2-0 Ndanda
Simba 2-2 Yanga

Mapinduzi Cup
Simba 3-1 Zimamoto

Nusu fainali
 Azam 0-0 Simba
     2-3 Penalti

 Fainali
Mtibwa 1-0 Simba

 Ligi Kuu Bara
Mbao 1-2 Simba
Alliance 1-4 Simba

Kombe la FA 
Simba 2-1 Mwadui

Ligi  Kuu Bara
Simba 3-2 Namungo
Simba 2-0 Coastal
Simba 2-1 Polisi Tanzania
Simba 0-1 JKT Tanzania

KOMBE LA SHIRIKISHO
Mechi 2
Shinda 2
Sare 0
Poteza 0


%%%%%%

KOMBE LA MAPINDUZI

Mechi  3
Shinda 2
Sare 0
Poteza 1

%%%%%%

LIGI KUU BARA:
Mechi 10
Shinda 8
Sare 1
Poteza 1

%%%%%%%%%%%%%

ZOTE JUMLA :
MECHI  15
SHINDA 12
SARE 1
POTEZA 2



SOMA NA HII  MSIMAMO WA LIGI KUU TANZANIA BARA UPO NAMNA HII