Baada ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kukutana katika kikao chake cha Februari 10, 2020. Imefikia hamuzi wa kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya uamuzi ufuatao;
Mechi namba 191: Simba SC (0) vs JKT Tanzania (1)
Mwamuzi msaidizi namba mbili Kassim Mpanga amefungiwa miezi mitatu(3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria za mpira wa miguu katika mechi iliyochezwa Februari 07,2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni namba 39(1) ya Ligi Kuu Kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Pia katika kikao hicho Kamati iliielekeza Sekretarieti kufuatilia viongozi wa vilabu na Makocha ambao hivi karibuni wamekuwa wakishutumu na kutoa matamshi yenye kukashifu na kudhalilisha viongozi,Chapa (Brand) ya Ligi na Taasisi kwa ujumla kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa vipindi tofauti tofauti.
Viongozi na Makocha waliobainika ni wafuatao Kocha wa Klabu ya Namungo FC (Hitimana )-kwenye mchezo wa Simba SC na Namungo Fc, Kocha wa Klabu ya Young African Sc (Luc Aymael)-kwenye mchezo wa Yanga Sc na Lipuli, Msemaji wa Klabu ya Simba SC (Haji Manara) na Muhamasishaji wa Young African sc(Anthonio Nugaz) .
Kutokana na matamshi hayo wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF).
Ligi Daraja la Pili:
Mechi namba 19C : DTB Fc 1 vs Tukuyu Stars 0
Klabu ya DTB iliomba marejeo kuhusiana na mchezo huo na Kamati imepitia na kukubaliana na utetezi wao hivyo matokeo yatabaki kama yalivyokuwa.