Kocha wa zamani wa Yanga, raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera amekiri wazi kuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Benard Morrison ni bonge la mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufanya chochote ndani ya uwanja kwani anaamini angekuwa wakati yake Yanga isingepata tabu.
Zahera ametoa kauli hiyo baada ya kumuangalia nyota huyo raia wa Ghana aliyejiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili akitokea Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambapo mpaka sasa ameshafanikiwa kufunga mabao mabao matatu na kutoa asisti mbili ndani ya timu hiyo.
Zahera alisema kiungo huyo ana uwezo mkubwa wa kucheza akitokea pembeni na amekuwa msaada kwenye timu hiyo tofauti na wakati wake kwani alikosa wachezaji wa aina hiyo.
“Unakumbuka nilikuwa nawaambia kwamba wakati wangu nilikosa wachezaji wenye uwezo wa kutokea pembeni na akafanya kila kitu ndani ya uwanja sikuweza kupata lakini sasa unaona kila mmoja amekuwa akimsifia.
“Amekuwa akiifanya kazi yake vizuri, anaingia na mipira ndani ya eneo la hatari anapiga chenga, akipokonywa mpira unaona kabisa anatafuta, hivyo ndiyo mchezaji anatakiwa kuwa naamini ana nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vyema Yanga,” alisema Zahera.