MIKEL Arteta, Kocha Mkuu wa Arsenal amesema kuwa alipata mshtuko baada ya kupata habari kwamba Manchester City imefungiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwa mipango yao ni kupambana kufikia malengo yao bila kutegemea mteremko.
Arteta alifanya kazi na Pep Guadiola ndani ya Manchester City akiwa ni msaidizi wake kwa muda wa miaka mitatu na nusu wakiwa ndani ya Etihad na sasa yupo Arsenal na alikiongoza kikosi chake kushinda mabao 4-0 mbele ya Newcastle mchezo wa Ligi Kuu England ikiwa ni ushindi wake wa kwanza ndani ya mwaka mpya 2020.
Wiki iliyopita City walifungiwa kutoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Uefa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa wamekiuka masharti ya masuala ya matumizi ya fedha kwenye usajili na adhabu hiyo ni ya miaka miwili.
Arteta amesema:’Sifikirii kuhusu wao kufungiwa kwamba kwetu itakuwa ni rahisi ama kutupa faida, hapana, nilipopata taarifa hizi jambo la kwanza nilishtuka nilifanya mawasiliano na Pep kupitia simu pamoja na viongozi wa City kwani najua kwa sasa wanapitia kipindi kigumu,”.