OLIVER Giroud na Marcos Alonso leo wamepeleka furaha ndani ya kikosi cha Chelsea baada ya kuichapa mabao 2-1 timu ya Tottenham iliyo chini ya Jose Mourinho kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.
Chelsea iliyo chini ya Frank Lampard ambaye ni Kocha Mkuu wa timu hiyo ilianza kwa spidi kuliandama lango la Spurs na kwenye kosakosa tatu za hatari dakika ya 15 walipata bao la kuongoza lililojazwa kimiani na Giroud.
Mpaka wanakwenda mapumziko, Chelsea walikuwa mbele kwa bao hilo na dakika tatu mbele walipachika bao lingine la pili lililowamaliza nguvu wapinzani wao Spurs lililofungwa na Alonso dakika ya 48 kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Spurs.
Bao la kufutia machozi kwa Spurs lilipatikana dakika ya 89 kwa mchezaji wa Chelsea Antonio Rudiger kujifunga kwenye harakati za kuokoa hatari ndani ya lango lake.
Spurs imepoteza mechi zote mbili ilizokutana na Chelsea ule wa kwanza wakiwa nyumbani walichapwa mabao 2-0 na leo wamechapwa mabao 2-1.
Ushindi huo unaifanya Chelsea kuwa nafasi ya nne na pointi zake 44 huku Spurs ikiwa nafasi tano na pointi 40 zote zimecheza mechi 27.