Na Saleh Ally
GUMZO la Dabi ya Kariakoo limerejea tena, kila mmoja anajua anachokiamini na anazungumza anachoona ndio sahihi.
Nani atashinda? Ni suala lenye maswali mengi ambayo kawaida huwa hakuna uhakika wa majibu lakini takwimu zinaweza kuwa na nafasi ya kwanza kutengeneza njia ya kuangalia mchezo ukoje.
Kikubwa mchezo wa Dabi, hasa hii ya Kariakoo huwa unashangaza kwa kuwa wakati mwingine hata takwimu nazo zinapigwa bao kutokana na ugumu wenyewe wa mchezo.
Pamoja na kwamba takwimu za nyuma wakati mwingine zinashindwa kuweka wazi mwendo wa Dabi ya Kariakoo inavyokuwa, lakini hauwezi kuzikwepa wakati unapozungumzia ujio wa mchezo huo.
Angalia mechi tano zilizopita za Yanga ambao watakuwa wenyeji lakini mechi tano za Simba watakaokuwa wageni utagundua kuna jambo na linaweza likawa linaashiria kuwa hautakuwa mchezo laini.
Nasema hautakuwa mchezo laini kwa maana ya kupata matokeo kwa wepesi ingawa kweli, inawezekana kuwa na matokeo ya kushangaza.
SIMBA:
Takwimu za mechi 5 zilizopita kwa upande wa wageni Simba zinaonyesha hivi; wameshinda zote 5 na kukusanya pointi 15.
Katika mechi hizo tano, Simba wamefunga mabao 10 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu tu.
Kama utafanya tathmini za karibu katika mechi tatu za mwisho, Simba pamoja na kufunga mabao mengi, nyavu zake zimeguswa zaidi ya Yanga.
Katika mechi hizo tatu, Simba imefunga mabao nane na kuruhusu matatu.
YANGA:
Kwa upande wa Yanga, katika mechi zao tano wameshinda mbili tu wakitoa sare mechi tatu na kukusanya pointi tisa.
Yanga wamefunga mabao matano na kuruhusu bao moja tu la kufungwa.
Ukifanya tathmini ya mechi tatu za mwisho, Yanga imefunga mabao manne na haikufungwa hata bao moja. Ilikutana na Coastal ikawa sare ya 0-0, mechi mbili za mwisho ikashinda 2-0 kila mechi dhidi ya Alliance na Mbao.
Kipimo cha mwisho unaona Yanga ina safu bora ya ulinzi katika mechi hizi tatu na baadaye tano za mwisho kutokana na kuruhusu mabao machache ya kufunga.
Safu ya ulinzi ya Kelvin Yondani na Lamine Moro pamoja na Jaffary Mohammed na Juma Abdul iko vizuri zaidi katika kutoruhusu mabao.
Kazi ya safu ya ulinzi ya Luc Eymael imeimarika zaidi na ngumu kufungika lakini inakutana na safu kali zaidi ya ushambulizi katika Ligi Kuu Bara.
Safu ya Meddie Kagere, Luis Miquissone, Cletous Chama na John Bocco ni hatari zaidi na unaona namna wanavyokwenda wakiwa wamefunga mabao 55 katika mechi 26 na Yanga katika mechi 24, wao wamefunga mabao 29.
Ukisema uangalie kwa ujumla, kidogo inaweza ikakupoteza zaidi kwa kuwa safu ya Simba inaonekana ni ngumu zaidi kwa kufungwa mabao 14 tu na Yanga kuruhusu mara 18.
Ndio maana nikasisitiza, vizuri kuangalia katika hizo mechi tano au tatu zilizopita kwa kuwa zinaonyesha kazi ya makocha wote akiwemo Eymael ambaye hata mechi ya kwanza ya Dabi ya Kariakoo, hakuwa ameanza kazi Yanga.
Katika soka kama nilivyoeleza awali, takwimu ni nzuri kutengeneza mwelekeo kwa maana ya mwendo wa mechi inayofuata lakini bado haziwezi kuwa mwamuzi wa kila kitu.
MECHI 5 ZA SIMBA LIGI KUU
Lipuli 0-1 Simba Samora
Simba 1-0 Kagera Taifa
Simba 3-1 Biashara Taifa
Simba 2-0 KMC Taifa
Azam 2-3 Simba Taifa
MECHI 5 ZA YANGA LIGI KUU
Yanga 0-0 Prisons Taifa
Polisi 1-1 Yanga Ushirika
Coastal 0-0 Yanga Mkwakwani
Yanga 2-0 Alliance Taifa
Yanga 2-0 Mbao Taifa