BAKARI Shime, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake ameshuhudia vijana wake chini ya miaka 17 wakipoteza kwa kichapo cha mabao 5-0 mbele ya Uganda kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia kwa Wanawake.
Kombe hilo linatarajiwa kufanyika nchini India mapema mwaka huu na litakuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zenye uwezo kupenya hatua zinazofuata.
Tumeona mchezo wa kwanza Tanzania ikiwa Uwanja wa Taifa ilishusha kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Uganda na iliambulia ushindi huo ikiwa kwenye ardhi yake ya nyumbani.
Faida ya Uwanja wa nyumbani na hasara za kushindwa kutumia vema uwanja wa nyumbani tumekuja kuzipata baada ya mchezo wa pili ambao unaamua mshindi nani atapenya hatua inayofuata.
Kila siku nimekuwa nikishauri inapopatikana nafasi ya kushinda kwenye mchezo wa nyumbani ni lazima kazi imalizike mapema ili mchezo wa pili uwe wa kukamilisha hesabu.
Kichapo cha mabao 5-0 kiwe somo kwa mechi zinazofuata na kuwaandaa vema wachezaji kisaikolojia kutumia vizuri faidia ya mashabiki na uwanja wa nyumbani kushinda kwa mabao mengi.
Watoto wamepambana kusaka ushindi mwisho wa siku wameambulia kichapo cha mabao 5-0 na kuwafanya watolewe kwenye mashindano kwa zigo la mabao 6-2 hapa pana kitu cha kujifunza na sio kulaumu.
Nimeona Shime anaingia kwenye mtego wa kulia na wachezaji waliocheza ndani ya Uganda hiyo ni pata potea na soka letu Afrika Mashariki tunalijua namna lilivyo na zengwe hilo halitupasi tuumize sana kichwa..
Kwa sasa Shime unapaswa ukizame upya kikosi chako makosa yalipojificha ili iwe kazi rahisi kupata matokeo kwenye mechi nyingine zinazofuata.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni wakati mwingine wa kuendeleza soka la Wanawake kushindwa kwa watoto hawa isiwe mwisho wa hesabu zinazofuata kwani wahenga walisema kuwa kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi.
Wahusika hawatazami kwa ukaribu kwani wengi wao wanalizwa huku na hakuna mtetezi wao kutokana na kutoonyeshwa kwenye TV.
Pia iwe somo kwa timu nyingine wakati mwingine kwenye mashindano ya kimataifa kwenye mechi tutakazopata nafasi kuanzia nyumbani kukazana kupata ushindi wa mabao mengi yatakayotufanya tuwe salama.
Pia kuna umuhimu wa kukumbuka kwamba wanafamilia ya michezo kwa sasa kuna umuhimu wa kuongeza umakini katika yale tunayoyafanya kutokana na uwepo wa virusi vya Corona ambavyo vimeleta hofu kwa dunia nzima.
Tusipuuze mambo tukidhani kwamba hayatuhusu hiyo sio tabia ya wanamichezo ni suala letu sote tuwaombee ndugu zetu wanaoumwa na wale ambao wapo kwenye nchi ambazo zinaathirika na ugonjwa huo.
Tusisahau kwamba Tanzania sio kisiwa ni nchi na masuala yanayotokea duniani yanatuhusu nasi pia ni wakati wetu kuendeleza utamaduni wetu wa kuwaombea ndugu zetu huku nasi tukichukua tahadhari kwani tayari Virusi vimeshafika nchini muhimu kujilinda na kuondoa hofu.