MAMBO yanapozidi kuwa magumu inaelezwa kuwa kuna wepesi unakuja huu msemo upo kila siku kwenye maisha ila ukiutumia kwenye michezo unapotea jumlajumla.
Kwa sasa Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa muda wa mwezi mmoja ili kutoa muda wa kupambana na virusi vya Corona ambavyo vimeanza kusambaa duniani.
Corona imekuwa ikisambaa kwa binadamu kwa njia ya hewa kwa mujibu wa wataalamu ambapo kasi yake inahusisha majimaji.
Kwa mujibu wa Dr.Maro ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Memorial Hospital amesema Virusi vya Corona vinaingia kwenye mwili wa binadamu kupitia njia ya hewa na vikiingia ndani mwili huathiri mfumo wa hewa.
Tahadhari inabidi ichukuliwe kwa kufuata kanuni za afya ili kuendelea kuwa salama na kupunguza hofu kwani hofu pia ni adui mkubwa kwenye kupambana na ugonjwa huu.
Kwa upande wa ligi ilikuwa inazidi kumeguka taratibu huku Ligi Daraja la Kwanza na la pili ilikuwa ikipamba moto.
Kuna mambo ambayo yalikuwa yanatokeo ndani ya ligi zote utafikiri wachezaji na waamuzi wote mwalimu wao ni mmoja jambo ambalo halileti afya kwenye soka letu.
Wakati timu za Ligi Kuu Bara zinahaha kujinusuru kutoshuka daraja tayari kuna kampeni za kila mmoja ashinde mechi zake jambo ambalo halileti maendeleo ya soka.
Mbeya City iliyo nafasi ya 17 ikiwa na pointi 30, Alliance ipo nafasi ya 18 ikiwa na pointi 29 hizi mbili zimecheza mechi 29 kwenye ligi na zina mechi tisa mkononi kwa sasa.
Mbao nafasi ya 19 ikiwa na pointi 22 imebakiza mechi 10 baada ya kucheza mechi 28 huku Singida United ikiwa nafasi ya 20 na pointi zake 15 ikiwa imecheza mechi 29 ina mechi tisa mkononi.
Hizi timu nne zote zipo nafasi nne za mwisho na ikiwa zitashindwa kupiga hesabu vizuri basi mkono wa kwa heri unazihusu kutokana na ukweli kwamba msimu huu zinashuka timu nne jumlajumla.
Mwenedo mzima wa ligi umekuwa na matatizo ya hapa na pale lakini hilo sio sababu ya kufanya timu zishindwe kujipanga na kupata matokeo mwisho wa siku kwa sasa timu zinahaha kujinasua kwenye mechi zao zilizobaki.
Kumekuwa na kampeni ya kwenye kanda ambazo zinahaha kujinasua kwenye hatua ya kushuka kufanya figisu ili kushinda mechi zao za nyumbani hili ni janga na linatakiwa kutazamwa kwa wakati.
Pia wakati haya yakitokea ndani ya Ligi Kuu Bara kwenye Ligi Daraja la Kwanza moto wao kila mmoja anataka apande daraja ashiriki Ligi Kuu Bara nao wanakwambia uwanja wa nyumbani hatoki mtu.
Kikubwa kinachotakiwa kufanyika ndani ya Ligi Daraja la Kwanza ni timu kupambana na waamuzi kufuata sheria 17 ili kuepuka haya mambo sio afya kwa soka letu.
Ganzi hii inaendelea mpaka ndani ya Ligi Daraja la Pili huku unaambiwa waamuzi wanafanya namna ambavyo wanajiskia wao na mashabiki wanaingia na matokeo uwanjani.
Tunaona kwamba hivi karibuni Toto Afrikan wamepeleka malalamiko kamati ya masaa 72 kutokana na kufanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana kwenye mechi tatu mfululizo.
Inaumiza kuona kwenye kiwanda cha kutengeneza wachezaji wajao hapo baadaye watakaoleta ushindani kunakuwa na madudu mengi ambayo ufuatiliaji wake bado una mwendo wa kobe.
Inatosha kwa sasa maumivu haya wanayoyapata wamiliki na mashabiki wa Ligi Daraja la Kwanza na la pili kupitia mateso makubwa kuzipandisha timu zao kwa mbinde kisha zikashindwa kuleta ushindani ndani ya ligi zikaangukia pua.
Kinachotakiwa ni timu zote kujipanga na kufuata namna kanuni zinavyotaka na hili litaongeza ushindani kwenye ligi zote na kufanya soka kuwa na ushindani.