KOCHA wa Simba, Sven Vanderbroeck amesisitiza kuimarika kwa mshambuliaji wake, Miraji Athuman ‘Sheva’, kutaifanya timu yake itishe zaidi kwenye eneo la mbele kwa vile Mnyarwanda Meddie Kagera atapata msaidizi wa kumwongezea nguvu.
Sven, ambaye aliweka wazi kwa sasa kikosi chake cha kwanza alichokuwa anakitumia, Kipa ni Aishi Manula, beki wa kulia Shomari Kapombe, beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Mabeki wa kati Muivory Coast Pascal Wawa na Erasto Nyoni, kiungo mkabaji Jonas Mkude, huku akiwataja Mzambia Clatous Chama, Mkenya Frances Kahata na Luis mbele, mastraika wake ni John Bocco na Mnyaranda Meddie Kagere.
Alisema, Kagere anahitaji msaidizi mbele na kuimarika kwa Sheva kunafanya liwe chaguo lake là kwanza kuifanya Simba kung’ara zaidi na kuendeleza rekodi zake za kubeba mataji.
“Mbali na usajili, mtu wa kwanza ninayemwangalia na kumtegemea kuongezea nguvu kikosi changu ni Miraji baada ya kuimarika,” alisema Sven.
“Miraji ndiye namtegemea kuja kuwasaidia Kagere na Bocco kwa sababu nafasi hiyo inauhitaji wa watu zaidi, kabla ya kuangalia wengine namoa nafasi yeye,” alisema Mbelgiji huyo.
Sheva anayesubiri kauli ya mtaalamu wa viungo Mtunisi Adel Zrane aanze mazoezi magumu baada ya kumaliza programu ya mazoezi viungo alisema;
“Binafsi nimejiandaa vizuri lengo ni kufanya kazi na sitawaangusha kikubwa waniombee.”
“Ninachoamini, kurudi kwangu kikosini na ushirikiano wa wenzangu tutaifanya Simba kuwa imara zaidi,” alisema Miraji.
Kocha Sven alikumbusha kwa kusema kufika kwao ilimlazimu kumtumia Kagere kwani Sheva na Bocco walikuwa majeruhi.
“Baada ya kuimarika kwa Bocco nikaona nibadilishe, ile ilikuwa ni kwa sababu,” alisema Sven.