MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Obrey Chirwa amesema ameamua kuiheshimu klabu yake kwa kutorejea kwao Zambia vinginevyo angeonekana mtovu wa nidhamu.
Chirwa raia wa Zambia mwenye asili ya Malawi amesema tangu Ligi Kuu Bara isimame hakuondoka nchini kama ambavyo wenzake wa kigeni wamefanya na kuamua kusalia jijini Dar es Salaam.
Chirwa amesema sababu kubwa ambayo imemfanya kutochukua uamuzi huo ni kwamba isingekuwa rahisi kurejea kwa muda mfupi kama angefika kwao.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga amesema kama angerudi kwao Zambia kisha kuanza kuangalia mambo yake binafsi yangemfanya kuwa katika nafasi ngumu kurudi nchini kumalizia msimu.
Amesema pia familia yake asingeweza kuiacha kwa muda mfupi na kwamba ameamua kubaki nchini kuepusha ugomvi na waajiri wake.
Aidha Chirwa amesema licha ya kubaki kwake nchini ameendelea kujifua mwenyewe kwa mazoezi mbalimbali akiwa pekee yake