Timu ya Arusha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Bara, kupitia kwa Ofisa habari wake Bahati Msilu wameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuta msimu wa Ligi Daraja la Kwanza 2019/20 kutokana na janga la Virusi vya Corona linaloendelea kuitikisa Dunia.
Msilu amesema:-“Ningefurahi kama ligi msimu huu ingehairishwa ili tuanze kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao kwani mapumziko haya ya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 yametuharibia utaratibu wote kwani yametusababishia gharama zisizokuwa za lazima maana tumetumia gharama ambazo hatukupaswa kutumia kulingana na hali mbaya ya timu yetu kiuchumi tuliyonayo”.
Msilu aliendelea kwa kusema kama TFF wataruhusu ligi iendelee basi watoe walau wiki mbili za kujipanga kila mchezo kutokana na hali mbaya kiuchumi.
“ TFF kwa msimu huu wa 2019/20 wangeacha tujiandae kwa msimu ujao, ligi ikiendelea ushindani utakuwa mdogo kwakuwa wachezaji wengi hawana nidhamu ya kufanya mazoezi watarudi wakiwa wazito ukichanganya na janga la Covid-19 hali ya uchumi imekuwa ngumu” , amesema.
Chanzo: Championi