Home Uncategorized SIMBA SC YAKOMBA MABEKI WOTE STARS

SIMBA SC YAKOMBA MABEKI WOTE STARS

SIMBA ipo katika mawindo ya kuimarisha kikosi chake kwa msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa, endapo itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mawindo hayo, Simba inatarajia kufanya kufuru kubwa kwa kung’oa vifaa vyote hatari ndani ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Baada ya kudaiwa kumalizana na beki wa kati, Bakari Mwamnyeto ‘Nondo’, anayechezea Coastal Unioni, Simba imepanga kumchukua beki mwingine wa Tais Stars, Idd Mobby,  anayekipiga Polisi Tanzania.

Simba ilianza kumfuatilia Mwamnyeto tangu alipofanya vizuri katika mechi ya Taifa Stars dhidi ya Sudan na kufanikisha timu hiyo kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Katika mchezo huo ambao Taifa Stars ilishinda kwa mabao 2-1, Mwamyeto alitengeneza pacha nzuri na Erasto Nyoni, hali iliyowavutia viongozi wa Simba.

Hata hivyo inadaiwa kuwa kutokana na Nyoni na Wawa kutokuwa na muda mrefu wa kucheza katika kikosi hicho, uongozi umeanza kuweka mikakati mapema kwa kufanya usajili wa mabeki wapya ili waanze kuzoeana.

Kwa taarifa ambazo gazeti la  DIMBA imezipata kutoka ndani ya Simba, inadaiwa katika mapendekezo ya kuimarisha nafasi hiyo ya ulinzi, Seleman Matola ambaye ni kocha msaidizi, ndiye alipendekeza usajili wa Mobby.

Ikumbukwe Matola ndiye alimsajili Mobby katika kikosi cha Polisi Tanzania akitokea Mwadui FC, hivyo uwezo wake umemshawishi kumvuta Msimbazi.

Beki huyo ni muhimili katika kikosi cha Polisi Tanzania, kwani hajawahi kukosa mechi msimu huu au kukaa benchi, labda awe majeruhi. Pia amekuwa katika timu ya Taifa Stars tangu Etienne Ndayiragije, raia wa Burundi, akabidhiwe mikoba kutoka kwa Mnigeria Emmanuel Amunike.

“Ukiachana na Mwamnyeto, Simba inachukua beki mwingine wa Taifa Stars, yule anayecheza Polisi (Mobby), lengo ni kuwaandaa wachezaji hao kurithi mikoba ya Nyoni na Wawa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Baada ya taarifa hizo kuzangaa, gazeti la DIMBA lilimtafuta Mobby jana na kukiri kufuatwa na Simba, lakini amesema bado mazungumzo rasmi hayajaanza.

SOMA NA HII  TUENDELEE KUCHUKUA TAHADHARI TUINGIAPO UWANJANI ILI BURUDANI IENDELEE

“Ni kweli Simba niliongea nao, lakini mambo bado hayajafikia katika makubaliano kwa sababu nina mtakaba na Polisi Tanzania,” alisema.

Alifafanua kuwa mkataba wake na Polisi Tanzania unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo anasubiri hadi ufike ukingoni aondoke akiwa huru.

Wiki iliyopita Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema kati ya maeneo atakayofanyia kazi katika usajili ni mabeki wawili.