KWA Tanzania hakuna mchezo wa soka wowote ambao unaendelea kwa sasa na hii ni kutokana na janga la Virusi vya Corona.
Ligi Kuu Bara pamoja na ligi nyingine za madaraja tofauti kwa sasa zimesimama pamoja na michezo mingine kama kikapu, gofu na mashindano mengine.
Lakini hapa tukirudi kwa upande wa soka, licha ya uwepo wa janga la Virusi vya Corona ni vizuri wale ambao wanasimamia viwanja wakaendelea kuvitunza.
Utamu wa soka siku zote hupendeza zaidi pale pitch inapokuwa katika ubora na majukwaa kuwa katika hali nzuri na si vinginevyo.
Kwa kuwa kipindi hiki hakuna soka licha ya uwepo wa Virusi vya Corona, lakini inatakiwa viwanja vya soka vikatunzwa kwa umakini mkubwa ili pale ligi itakaporejea kusiwepo sintofahamu.
Kiuhalisia ni kwamba Tanzania kwa asimilia 90 haina viwanja bora vya soka hasa vyenye nyasi za asili na ubora unaozungumziwa hapa ni ule wa Uwanja wa Taifa wa jijini Dar es Salaam.
Hivyo ni vizuri vyombo vya soka kupitia wasimamizi wake wakuu, Bodi ya Ligi wahakikishe kuwa viwanja vyote ambavyo hutumika kwenye ligi viwe katika hali nzuri pale ligi itakaporejea.
Sababu kipindi kama hiki maeneo mengi ni masika hivyo ni vizuri kujua ni kitu gani kimo ndani ya viwanja hivyo kwa maslahi ya soka.