Yanga hivi sasa wanasubiria tu dirisha la usajili lifunguliwe, kwani tayari kibindoni wana kitita Sh Bil 1.5, ambazo wametengewa na wadhamini wao Kampuni ya GSM.
Tayari wana orodha ya baadhi ya wachezaji wanaowahitaji watakaokuja kuchukua nafasi za nyota ambao wameshindwa kutoa mchango katika timu hiyo.
Wapo baadhi ya wachezaji waliokuwepo kwenye mazungumzo nao watakaokuja kuichezea timu hiyo kwenye msimu ujao ambao wanaonekana kuwa watabadilisha rasmi kikosi cha Yanga.
Pamoja na kwamba Yanga wanatajwa kuwa wanaweza kusajili wachezaji na wenye majina makubwa, lakini waliopo hapo chini wanaonekana kuwa watakuja na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja:
Heritier Makambo- Horoya AC
Huenda ukawa usajili wa kwanza ndani ya Yanga ni kutokana na kuwa mshamnbuliaji kipenzi cha timu hiyo ambaye akiwa na Yanga msimu uliopita alifanikiwa kufunga mabao 17 katika ligi kuu.
Anakuja kuchukua nafasi ya Mkongomani, David Molinga, ambaye licha ya kuongoza kwa idadi ya mabao nane ndani ya timu hiyo katika ligi kuu, lakini anaonekana siyo chochote, yupo kwenye orodha ya wale wanaoachwa.
Kwa uhalisia Makambo anakuja kuchukua nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Ally Niyonzima- Rayon Sport
Huyu kiungo mkabaji tegemeo wa Rayon anayemudu kucheza namba sita, atakuja Yanga kumpa changamoto ya ushindani Mkongomani, Papy Tshishimbi na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anahitaji kupambana ili kuhakikishia anamtoa kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kama akitua.
Huyu kwa jinsi hali ilivyo anaonekana kuwa anaweza kuwaweka wote nje, moja ya sakata la Tshishimbi la hivi karibuni la kutaka kuondoka linaweza kumfanya kocha akafikiri kumtumia Niyonzima zaidi.
Michael Sarpong- Mchezaji Huru
Huyu mkataba wake umevunjwa na mabosi wa Rayon Sports ya Rwanda, ana kibarua kigumu cha kumuondoa Ditram Nchimbi ambaye kipenzi cha Wanayanga na kocha Eymael kutokana na kiwango kikubwa ambacho alikionyesha tangu alipotua kwenye timu hiyo katika dirisha dogo msimu huu.
Ingawa ni muda utaongea zaidi kutokana na jinsi anavyotajwa kuwa mtu hatari, ana mudu kucheza namba kumi na wakati mwingine namba tisa, inaonekana kuwa anaweza akawa anapata namba kwenye moja kati ya nafasi hizo.
Mussa Mohammed- Nkana FC
Yeye anapambanishwa na Mghana, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Andrew Vicent ‘Dante’ na beki wa kati kipenzi cha kocha Eymael, Juma Said Makapu, ambaye tangu kocha huyo ametua kukinoa kikosi hicho amekuwa chaguo lake la kwanza.
Mussa anatajwa kuwa ni kati ya mabeki bora wa kati wa Ligi ya Zambia, hivyo kama akitua ataiboresha vema safu hiyo ya ulinzi ya kati ambayo kocha huyo amekuwa akilalamimikia kutokana na kuruhusu mabao mengi ya kizembe.
Tuisila Kisinda – AS Vita
Ni kati ya mawinga bora hivi sasa huko DR Congo, anacheza nafasi zote za pembeni, namba 7 na 11, ambayo hivi sasa inachezwa na Bernard Morrison pale Yanga.
Huyu atapata ushindani kutoka kwa Nchimbi ambaye Eymael amekuwa akimtumia mara kadhaa namba 7, licha wakati mwingine kumtumia straika namba 9. Kwa ujumla anaonekana kuwa hawezi kufua dafu kwa Morrison ambaye ameshajihakikishia namba Yanga.
Yassin Mustapha – Polisi Tanzania
Huyu ni beki wa kushoto ambaye atakutana na changamoto kubwa kutoka kwa Jaffar Mohammed aliyebadilishiwa majukumu ya kucheza nafasi hiyo kutoka kiungo hadi beki. Msimu huu ameonyesha kiwango kikubwa.
Inaonekana kuwa Jafarry atarudishwa akapambanie namba yake huko mbele na kumuacha Yassin hapa.
Wachezaji ambao hata kama wakisajiliwa hawataleta ushindani mkubwa wa namba ni Reliants Lusajo (Namungo FC), Dickson Job (Mtibwa Sugar), Said Ndemla (Simba), Abdulhalim Humud (KMC) na Sven Yidah (Kariobang Sharks).
SOURCE: CHAMPIONI