MTENDAJI Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema kuwa mashabiki wa Simba wanatakiwa wawe watulivu kuhusiana na usajili wa wachezaji wapya ndani ya timu hiyo, kwani uongozi unafahamu nini unafanya.
Senzo aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya maandalizi ya Kombe la Dunia lililofanyika nchini Afrika Kusini 2010, anakuwa kiongozi wa kwanza raia wa Afrika Kusini kuwa mtendaji mkuu wa Simba.
Senzo amesema kuwa wanafahamu kuwa mashabiki wa Simba wanatamani kuona kila mara timu ikifanya usajili ili timu iwe bora hivyo aliwaambia watulie kwani uongozi wa timu hiyo, upo makini katika masuala ya usajili ili kuhakikisha inazidi kuwa bora.
“Mashabiki siku zote wanataka kuona timu ikisajili kila baada ya dirisha kufunguliwa wakiamini timu bila kusajili haitafanya vizuri, sitaki kusema kuwa hatutasajili ila mipango yote ya kuhakikisha timu inakuwa bora ipo kwa viongozi ambao tunashirikiana kwa ukaribu na benchi la ufundi.
“Hakuna kiongozi wala benchi la ufundi la timu ambalo lipo tayari kuona timu haifanyi vizuri, hivyo malengo ambayo siku zote kila Mwanasimba huyatamani kuyapata haswa yale ya kimataifa ambayo bado hayatimia,” alisema kiongozi huyo.