MWANGA umeanza kuonekana kwa sasa kidogo kule ambako tunaelekea kutokana na vita ya Virusi vya Corona kuendelea kupamba moto.
Tayari tumeona kwamba yale maombi na dua za watanzania wegi kuhusu janga hili yakijibu kwani Serikali imesema kuwa maambukizi yameanza kupungua.
Ni kweli inaumiza pia ilikuwa inahuzunisha kuona kwamba kila siku hali inazidi kuwa tete na hakuna mwanga wa kufanikiwa katika hili jambo ambalo lilikuwa linawaumiza wanafamilia ya michezo pamoja na watu wengine kiujumla.
Kwa wakati huo hatukuwa na namna ya kufanya zaidi ya kuchukua tahadhari kwani Virusi vipo na mapambano ni lazima ilibidi yaendelee na hatimaye majibu yameanza kuonekana kwa sasa.
Haina maana kwamba kwa hatua ambayo tumefikia sasa ndiyo mwisho wa mapambano hapana ni lazima mapambano yaendelee mpaka pale hali itakapokuwa shwari kabisa mtaani.
Tanzania yetu na dunia nzima kiujumla inapambana kutafuta suluhisho la Virusi vya Corona kwani hakuna Serikali inayopenda kuona watu wake wakiangamia.
Kwenye familia ya michezo mambo yalikuwa bado hayajakaa sawa na matumaini yalipotea kabisa ila kwa sasa taratibu imani inaanza kurejea.
Ni ngumu kuamini kwamba mambo yamebadilika ila kweli habari ndio hiyo na ni lazima tuipokee ili tuitendee kazi kwa ukamilifu na hata mambo yatakaporudi kwenye hali ya kawaida ni lazima tujipange kiukweli.
Bado rai yangu ipo kwa watanzania kuwaomba wazidi kuchukua tahadhari na kuongeza umakini katika kupambana na Virusi vya Corona kwani naona wengi wameanza kupuuzia kwa sasa.
Ukubwa wa tatizo lililo mbele yetu sio wa kutisha ila ni lazima tujitoe kupambana kupata njia ya kutoka ili kila mmoja awe salama asiwe kwenye hatari kisa ameskia maambukizi yamepungua.
Wapo ambao wanapenda kuchukua taarifa ambazo sio sahihi na kusambaza kwa wengine kwa lengo la kutishana hii naona sio sawa.
Kwa hawa wenye tabia hii ikiwa wapo kwenye familia ya michezo wanapaswa wabadilike na wafuate miiko iliyopo kuhusu kutoa taarifa kuna mamlaka husika ziachwe zifanye kazi yake..
Ni janga ambalo linahitaji umakini mkubwa katika kupambana nalo na kutafuta majibu ya tatizo ambalo lipo kwa sasa.
Wote tunapaswa tuungane wote kupambana na Virusi vya Corona imani yetu ni kwamba hali itarejea kuwa salama tuzidi kuchukua tahadhari na kupambana kwa umoja wetu.
Wahenga walisema kwamba kidole kimoja hakivunji chawa hawakukosea walikuwa wana maana kubwa katika kuzungumzia hili.
Kwenye ulimwengu wa michezo ligi nyingi zinatarajiwa kurejea hivi karibuni na wengine wapo ambao walipewa mataji yao huku wengine wakifuta kabisa ligi.
Hiyo sio mbaya kwani kila mmoja ana namna yake ya kutatua matatizo ambayo anakabiliwa nayo sio swala la kuiga kila jambo hapana muhimu kutazama mbinu ambayo unaitumia kwenye kutatua tatizo.
Tusisahau kwamba kuna dalili njema za ligi yetu pia kuweza kurejea hivyo ni wakati mwingine wa kuona namna gani kutakuwa na maandalizi ya awali kabla ligi haijaanza.
Muhimu kwa wachezaji kuanza kujiweka sawa kisaikolojia ili ligi itakaporejea wawe kwenye utimamu wa akili na mwili pia kwenye ushindani wa soka.
Viongozi wa timu na mashabiki ni wakati wa kujiaandaa kuzirejesha timu pale ambapo zilikuwa awali kwa maana ya sapoti pamoja na mipango mipya ya kumaliza mzunguko wa pili.
Ukiachana na masuala ya kulinda vipaji pia kwa sasa kumekuwa masuala ya timu kufanya tathimini ya pale ambapo zilikwama kabla ya ligi kusimama.
Hili pia lisipuuzwe lifanywe kwa umakini lakini tahadhari pia ichukuliwe katika kujilinda kwani ligi ipo mlangoni inapiga hodi mambo yataanza muda sio mrefu.
Tusifikiri kwamba tupo salama kiasi kikubwa hapana ni Mungu tu anatufanyia amani hivyo nasi tuendekee kuomba dua ili tubaki salama na maisha yaendelee bila maumivu makubwa.
Muda wa kutengeneza ripoti maalumu ambazo zitakuwa mwongozo kwa ajili ya wakati ujao ndio unameguka hivyo kama ilikuwa bado ni lazima ukimbazane na muda.
Itapendeza kuona kwamba kila mwanafamilia ya michezo kwenye timu akitoa mchango wake na kusikilizwa kwa umakini ili kujenga umoja ndani ya klabu.
Kila mwanafamilia aanze kujiaandaa kisaikolojia kuhusu kurejea kwa ligi na ile itakayokuwa na ushindani bila kuwa na mashabiki kwani ni muhimu kuchukua tahdahari dhidi ya Corona.
Kile ambacho kinafikiriwa kwa sasa ni namna gani ligi itarejea na hatma yake itakuaje lakini katika hili tusiumize sana kichwa tunachotakiwa kuumiza kichwa chetu ni kwenye dua hali iwe salama.
Tayari Serikali imeanza kurejesha imani na kukubali kwamba kuna haja ya kurejesha ligi ili mambo yaweze kwenda kama ilivyokuwa zamani.
Hakuna ambaye hajakumbuka maisha ya ushindani kwenye Ligi Kuu Bara, Ligi ya Wanawake Ligi Daraja la Kwanza ilikuwa ni moto ambao unaendelea ila hakuna namna ya kufanya kwa sasa.
Tangu Machi 17 mpaka leo ni muda mrefu umepita bila kuona shughuli za michezo ila yote ilikuwa ni lazima iwe hivyo kutokana na janga la Corona.
Mamlaka husika kwenye masuala ya michezo Tanzania ambao ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni wakati wa kuona namna gani ligi itakamilika kwani muda uliobaki ni mchache.