Home Uncategorized MASUALA YA MICHEZO YANARUDI NI JAMBO JEMA, TUSISAHAU CORONA BADO IPO

MASUALA YA MICHEZO YANARUDI NI JAMBO JEMA, TUSISAHAU CORONA BADO IPO

IMESHAKUWA wazi kwamba masuala ya michezo yanarejea Juni Mosi baada ya Serikali kuruhusu burudani kuendelea baada ya kusimama kwa muda mrefu.
Machi 17 Serikali ilisimamisha shughuli za mpira kutokana na janga la Virusi vya Corona ambalo limeivuruga dunia hivyo ilikuwa ni muhimu kwa ajili ya kuchukua tahadhari.
Maisha yalikuwa yana tofauti yake kwani kukosa burudani ya mpira ilikuwa ni ngumu kwa mashabiki na wanafamilia ya michezo kuweza kuiweka akilini hali hiyo.
Ila hakukuwa na chaguo kwani janga la Corona lilikuwa linaitikisa dunia na ili kujilinda ilikuwa lazima kuchukua tahadhari kwa kupambana na Corona kwanza huku tahadhari zikiendelea kuchukuliwa.
 Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, aliamua kuwaomba watanzania wafanye maombi bila kuchoka na kuendelea kuchukua tahadhari.
Kutokana na hali hiyo hatimaye ameweza kuruhsu masuala ya michezo kuendelea kutokana na kuona kwamba hali imekuwa shwari kwa kiasi chake.
Kwa hatua ambayo Serikali imeamua kufanya inapaswa ipongezwa kwani imerejesha burudani kwa familia ya michezo na kuona namna gani burudani itaendelea.
 Kikubwa ambacho kinatakiwa kufanyika kwa sasa ni kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata yale maagizo ambayo tutapewa na mamlaka husika.
Kuna utaratibu ambao utatolewa na mamlaka unapaswa ufuatwe hilo lipo wazi kwani afya ni muhimu kwa kila mmoja kuwa salama.
Hatujui maradhi yatakuwepo ama yataisha lina kwa sasa zaidi tunachotakiwa kuendelea kuomba kwa Mungu wetu kila mmoja kwa imani yake ili haya yapite.
Tunatambua kuwa mamlaka ya Serikali imekuwa ikitupa taarifa kwamba hali imeanza kuwa shwari lakini bado wanatusisitiza tuchukue tahadhari kwani bado janga halijayeyuka kabisa.
Ulimwengu wa soka ambao ulikaa kimya tangu Machi 17 sasa Juni Mosi mambo yatakuwa hadharani na burudani itaendelea pale ilipoishia.
Muda mrefu umepita sasa tupo mwezi Mei tunazidi kuuyeyusha taratibu kuufukuzia mwezi Juni kwa mapenzi yake Mungu ni lazima tuendelee kushukuru huku juhudi zetu kuomba dua zikizidi kuwa kubwa bila kuchoka.
 Kwa muda huu ambao tunapitia tusijisahau na tukadhani labda mambo yamekwisha na kuendelea kuishi maisha yetu yale ya zamani hapana lazima tahadhari zichukuliwe.
Tahadhari zinazotakiwa kuchukuliwa hapa ni zile ambazo kila siku zinatolewa na Serikali yenyewe kupitia Wizara ya afya pamoja na wataalamu kuhusu utaratibu unaotakiwa kufanyika kwa wakati huu.
Hapa tunakumbushana kwani afya ni muhumi ndugu yangu msomaji ndio maana leo tunaendelea kuwa wazima kwa kuwa tuna utajiri wa afya ambayo tumepewa na Mungu.
Ukweli ni kwamba iwapo mtu yoyote atakuwa anafanya kinyume na utaratibu ili awe salama kwa kupuuzia ni rahisi kutokuwa salama.
Tusisahau kwamba idadi ya mashabiki imetolewa kwamba wasizidi 10 hilo ni la msingi kuzingatiwa tusianze kufanya ujanja katika hili na kupuuzia maagizo ambayo yanatolewa.
Hakuna shabiki ambaye hapendi kuona mpira lakini utaratibu uliowekwa kwa mazingira mabayo tunapitia ni lazima ufuatwe hatuna sababu ya kuanza kuwa wabishi ilihali ni kwa faida yetu.
Timu zinatazama mapato na kuvimbisha akaunti zao hilo lipo wazi lakini ni muhimu kutambua kwamba iwapo shabiki anayekupa mkwanja akawa na tatizo la kiafya kesho hawezi kuja.
Pia isitoshe kusema kwamba kwa sasa mechi ambazo zimebaki ni chache hazizidi 12 kwa timu zote ndani ya ligi hivyo ni muhimu kuangalia utajiri wa mashabiki wa kesho kuliko kuwatumia kwa sasa.
Ninarudia tena kwamba afya za mashabiki ni muhimu kuliko kiingilio chake ambacho atakiacha mlangoni kisha akawa kwenye hali ya maambukizi dhidi ya Corona.
Wizara ya afya pamoja na Serikali inajali afya za watu na inatambua kwamba nguvu kazi za watu zinategemea afya bora ambayo ni muhimu kulindwa kwa sasa.
Kwenye mpango wa kurejea ligi pia ni afya pia inahitajika kwani wachezaji hawawezi kucheza iwapo hawatakuwa na afya bora hata mashabiki hawataweza kushangilia iwapo hatakuwa na afya.
Utaratibu ulikuwa wazi tangu awali kwamba hakutakuwa na mashabiki hivyo timu zinapaswa zianze kuwa mabalozi kwa mashabiki wao kwa kuwapa taarifa sahihi na kutambua vigezo vya mashabiki ambao wanahitajika.
Mashabiki hao ambao hawazidi 10 ninaona kwamba kuna umuhimu wa kila timu kuweza kuwachagua mashabiki wao ambao watakuwa wanakwenda nao kwenye mechi zao.
Labda inaweza kuwa rahisi kwa kutafuta mashabiki wao ambao ni wale wanaopiga zile ngoma kwa kuzigawa mechi zao kimafungu kwani kwa sasa hakuna mechi nyingi zilizobaki.
Corona ipo tusijidanganye kwamba vita imekwisha hapana ni muhimu kuchukua tahadhari hivyo kwa upande wa mashabiki timu zinapaswa ziangalie ni namna gani zitawapata mashabiki wao.
Pia itapendeza iwapo mashabiki hao watapimwa Corona ili iwe salama kwao na wale ambao watakutana nao pale watakapokuwa ndani ya uwanja.
Tusisahau kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona ndugu zangu hili janga bado tupo nalo ni muhimu kujilinda kwa kuchukua tahadhari na kufuata kanuni za afya.
Mapato yapo tu siku zote hayawezi kuisha ila sasa kwenye afya hapo ndipo tatizo linapoanzia kwa kuwa afya ni muhimu kuliko mapato basi tukubali kukosa mapato na kulinda afya zetu.
Hii ni dharula isichukuliwe katika mfumo wa kisiasa kila mmoja akakubali kuwa ndani ya uwanja iwapo hana kibali ama kuwa karibu na uwanja kuwaona wachezaji.
Muhimu afya kuwa salama ili wakati ujao vita hii ya Corona itakapokwisha nawe pia uwe ndani ya uwanja ukicheka kwa kuwa umemshinda adui.
Maandalizi pia ni muhimu kwa sasa kwa timu ambazo zinakabiliwa na anguko la kushuka daraja zisijisahau zikadhani vita imekwisha.
Kikubwa wakati tunapambania afya zetu tukumbuke pia kupambania nafasi zetu ndani ya ligi ili pale mambo yatakapokuwa sawa ushindani uendelee.
Kwa kuwa kwa sasa  ligi ipo njiani kurudi basi kwa mchezaji ni lazima ajiwekee sawa kiakili kuamini kwamba atarejea uwanjani hivi karibuni.
Mwezi Juni unapiga hodi upo njiani kuja sio mbali ni karibu tu na kwa namna siku zinavyokwenda kasi ni lazima kila mmoja aanze kujipanga sawasawa.
Ninaamini kwa sasa muda ambao wamepewa utatosha kujiandaa kwani nina imani wachezaji walipewa program za kufanya ili kulinda vipaji.
Muda wa kuona burudani upo njiani hivyo ni muhimu kujiweka sawa na kujipanga kuendelea pale ambapo kazi ilikuwa imeishia wakati ule ligi inasimamishwa.
Ninaamini wengi wameanza kubadilika kwa kuchukua tahadhari na kufanya yale ambayo yanashauriwa na wataalamu wetu wa afya pamoja na Serikali kiujumla.
Wizara ya afya na Serikali katika hili pia wanastahili pongezi kwani taarifa zimekuwa zikitolewa mara kwa mara jambo ambalo linaongeza umakini.
Kanuni ni zilezile hazibadiliki kunawa mikono, umbali wa mita moja, kuvaa barakoa  ila kitu cha msingi hapa ni namna ya kuzifuata na kufanya kile ambacho kinaelekezwa na wataalamu wetu.
Unapozungumzia afya ni utajiri mkubwa ambao kila mmoja anapaswa kupambana kuwa salama yeye na wale ambao wanamzunguka kwa wakati uliopo kwa sasa.
Kwa wachezaji pamoja na viongozi pia ni muhimu kuendelea kuzifuata kanuni zile za afya ili kuendelea kuwa salama kwa wakati huu mgumu.
Kwa wachezaji ambao wanazipuuzia program ni wakati wao sasa kuonyesha kwamba wapo makini kwa kuanza kufanya muda huu ambao Serikali imeruhusu mazoezi kuanza.
Nina amini vita itakuwa kali hasa baada ya ligi kurejea kutokana na kila timu kupanga kufanya vizuri kwa mechi za mwisho ambazo zimebaki kwani kila mmoja anahitaji ushindi.
Tunatarajia kutakuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kuonyesha kwamba ilikuwa inastahili kupata matokeo mazuri yatakayowafikisha kwenye malengo yao.
Kazi kwa timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja zinapaswa zikazane kujiokoa ili msimu ujao ziwe ndani ya ligi.
Jambo la kuzingatia mamlaka husika za soka ikiwa ni TFF kuanza kuangalia ni namna gani mambo yanaweza kwenda sawa na kutoa taarifa kwa wakati ili timu zijiweke sawa.
Muda mchache ambao watapewa wa maandalizi ninaamini utatosha kuwarejesha kwenye ule mfumo wao ambao walikuwa wanauendeleza wakati ligi ikiendelea.
Zile zinazojipanga kupanda daraja ni lazima zitazame namna zitakavyoweza kwenda kwa kasi kwenye ligi iwapo zitapanda.
Jambo la msingi kwa sasa ni kila mmoja kuchukua tahadhari na kuamini kwamba ugonjwa upo na ligi ipo njiani kurudi maana wapo ambao walikuwa wamekata tamaa kuhusu kurejea kwa ligi.
Napenda kuwaomba kwamba kwa wakati huu kila mmoja awe balozi mzuri kwenye mapambano haya na tukishinda tushinde pamoja vita hii ambayo inasumbua vichwa vya wengi.
Muda wa maandalizi ambao utatolewa pia nao unapaswa utumike kwa umakini na tahadari ili kuendelea kulinda afya za wachezaji kabla ligi haijarejea.
Viongozi wa Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili ni lazima kuja na mkakati wa muda mfupi utakaotumika kumaliza mechi ambazo zimebaki.
Timu ambazo zinashuka ni nyingi hivyo vita itakuwa ni kubwa ndani ya uwanja kwenye kutafuta matokeo na hicho ndicho kinatakiwa.
Tuna kazi kubwa ya kushinda vita hii ya Corona inayovurugavuruga kila masuala kwa sasa inatosha kusema kwamba tuendelee kuchukua tahadhari ili kuwa salama.
Itatusaidia kuturejesha kwenye njia ambayo tulikuwepo awali wakati ule wa kushuhudia zile burudani ndani ya uwanja na tusipuuzie maagizo ambayo tunapewa.
Kikubwa kwa timu kuwa tayari kupambana ndani ya uwanja kutafuta matokeo chanya ambayo ni muhimu kwa kila mchezaji na timu kiujumla.
Bado ninapenda kuwaomba mashabiki kuendelelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona ambalo linaivuruga dunia.

SOMA NA HII  DAU LA KIUNGO ANAYEWINDWA NA YANGA ACHA KABISA, AKUBALI KUTUA