Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, ametuma ujumbe mzito kwa wapinzani wake Kagera Sugar ambao watacheza nao katika robo fainali ya Kombe la FA akiwaambia analihitaji kombe hilo kwa nguvu zote, hivyo atawafunga tu.
Kocha huyo amesema kwamba kile kilichotokea kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ambapo Yanga ilifungwa 3-0, hakitajirudia kwa sababu ya kulihitaji kombe hilo ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
Yanga na Kagera Sugar watapambana katika hatua ya robo fainali ya Kombe la FA ambapo mechi za hatua hiyo zimepangwa kupigwa kati ya Juni 27 na 28, mwaka huu jijini Dar.
Eymael amesema uzuri ni kwamba atakuwepo katika mechi hiyo na ana uhakika wa kuiongoza timu yake kushinda kutokana na mipango yake ya kuelekea kuchukua ubingwa huo.
“Nimepata taarifa za mechi hiyo na nimeona tumepangwa kucheza na Kagera Sugar. Najua katika mechi ya kwanza walitufunga lakini safari hii hawatusumbui, tutawafunga.
“Ujue hili kombe ndiyo nafasi kwetu sisi kucheza kimataifa na nishaweka mipango yangu ya kuhakikisha nalichukua, hivyo nasema kwamba kwa safari hii tutajiandaa kushinda dhidi yao.
“Uzuri ni kwamba hadi mechi hiyo inafika nitakuwa tayari nishafika Dar ingawa hadi sasa bado kuna changamoto ya usafiri wa ndege kutoka huku Ubelgiji, lakini naendelea kushughulikia kuona nakuja huko kuendelea na majukumu yangu,” alisema Eymael.
Wakati Eymael akisema hivyo, Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema: “Tumefurahi kukutana nao tena kwani tayari tumeshakutana mara moja na kuwafunga, hii ni nafasi nyingine ya kupata fursa ya kujijengea imani kwa mashabiki zetu kwa sababu najua tutawafunga tena kwa kuwa nafahamu jinsi ya kucheza nao.”
SOURCE: SPOTI XTRA