IMEELEZWA kuwa gharama ambazo amezitumia Kocha Mkuu wa Yanga kwa ajili ya tiketi mpaka sasa licha ya kutotua nchini ni zaidi ya milioni 40 zimeyeyuka kwa ajili gharama za tiketi pamoja na matumizi mengine.
Eymael kwa sasa yupo zake nchini Ubelgiji ambako alikwenda kwa ajili ya mapumziko baada ya Serikali kusimamisha masuala ya michezo Machi 17 kutokana na janga la Virusi vya Corona.
Hivi karibuni Eymael alilamika kuwa hajatumiwa tiketi na Uongozi wa Yanga jambo ambalo linamfanya aendelee kubaki Ubelgiji.
Tayari Serikali imeruhusu masuala ya michezo kuendelea kwa kueleza kuwa maambukizi ya Virusi vya Corona yamepungua na mechi ya Juni 13 Yanga itakuwa na kibarua cha kumenyana na Mwadui FC Uwanja wa Kambarage.
Habari kutoka Yanga zimeeleza kuwa:”Eymael ametumia gharama kubwa kwa ajili ya gharama za tiketi ikiwa ni zaidi ya milioni 40 pamoja na matumizi mengine, mara ya kwanza alisema kuwa ameshakamilisha utaratibu ilipwe tiketi kwenye kampuni ya Ethiopia ilipokamilishwa alibadili msimamo na kusema kuwa anaweza kuja na ndege nyingine itakayotua kati ya Juni 6 ama 7.
“Kumbuka kwamba katika hizo ndege GSM wanakamilisha malipo huku yeye akibadili mtazamo wake anavyotaka bila kuwafikiria waajiri wake, tena hata hiyo ya Juni 6 na 7 amebadilisha na amesema anaweza kuja Juni 17, gharama zote zinalipwa na GSM hili jambo limewakasirisha mabosi.
“Mbaya zaidi anatoa lugha ambazo sio nzuri kwa wahudumu wa ndege huko aliko pamoja na viongozi wa Yanga, amevuka mipaka mpaka ameingia anga za GSM sasa huyu mtu sijui anatarajia nini katika hili, iwapo atamaliza msimu salama ni jambo la kumshukuru Mungu,” ilieleza taarifa hiyo.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said hivi karibuni alisema kuwa utaratbu wa kocha kurejea unashughulikiwa na kuwataka mashabiki wasiwe na wasiwasi juu ya hilo.
“Kocha Eymael alikwenda Ubelgiji kwa ajili ya masuala ya ya kifamilia hivyo kwa sasa tunashughulikia suala lake atarejea hivi karibuni,” alisema.
Chanzo: SpotiXtra