LEO Uwanja wa Taifa kutakuwa na kazi moja kubwa kwa Simba iliyo nafasi ya kwanza na pointi 71 kuzisaka pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting iliyo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 39 baada ya kucheza mechi 28.
Ruvu Shoting itaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa ikiwa na kumbukukumbu ya kupoteza kwa kufungwa mabao 3-0 Novemba 23, Uwanja wa Uhuru.
Sven Vandenbroeck, Kocha Mkuu wa Simba, amesema kuwa wachezaji wake wapo tayari na wanachohitaji ni pointi tatu ili kujihakikishia nafasi ya kutwaa ubingwa.
Sven atakosa huduma ya majembe mawili ya kazi yaliyohusika kwenye jumla ya mabao 12 kati ya 63, Jonas Mkude mwenye mabao mawili na pasi mbili anaendelea na matibabu ya mguu na Sharaf Shiboub mwenye mabao mawili na pasi sita za mabao utaratibu wa kumrejesha kutoka Sudan alikokwenda baada ya janga la Corona unaendelea kwa kuwa mipaka kwao bado imefungwa.
Masau Bwire, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting amesema:”Tunataka kuwa kikwazo kwa wapinzani wetu, wamesema wanahitaji mechi nne ili kutwaa ubingwa, ila kwetu hakuna kitu hicho watuondoe kwenye timu nne wanazozitaja.
“Utapigwa mpira wa Barcelona mpaka wao washangae kwa nini wamekutana na sisi, ninajua wengi wanafikiri tutafungwa ila hilo halipo, tunataka ushindi na wachezaji wote wapo fiti.”