Home Uncategorized A-Z KUHUSU ISHU YA KAKOLANYA SIMBA IPO NAMNA HIVI

A-Z KUHUSU ISHU YA KAKOLANYA SIMBA IPO NAMNA HIVI

HALI ya hewa siyo nzuri baina ya kipa wa Simba, Beno Kakolanya na bosi wake, Mohammed Mwarami na inaelezwa wamechenjiana kwa maneno na ndiyo chanzo cha kusota jukwaani na mashabiki.

Tayari uongozi tangu jana umeanza kulivalia njuga sakata hilo na huenda pia leo wakawa na kikao kabla ya kuingia kambini kujiandaa na safari ya Mbeya.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba kipa huyo amekuwa hazungumzi lugha moja na Mwarami tangu timu hiyo ikiwa kambini nchini Afrika Kusini huku ikidaiwa kwamba kocha huyo amekuwa akisisitiza kuwa kijana wake amekuwa bonge.

Habari zinasema kwamba ishu hiyo ilikuwa mbaya zaidi baada ya timu kurejea kutoka kwenye mapumziko ya corona ambapo Kakolanya aliambiwa hayuko fiti na uzito wake umeongezeka jambo, lilimfanya kocha Sven kumuangalia kwa jicho la pili na kumpa mazoezi spesho kama kukimbia na kumgeuza refa wa wachezaji wenzake.

Habari zinasema kwamba Kocha Mwarami ameridhishwa na ubora wa kipa namba moja, Aishi Manula lakini akapendekeza kwamba chipukizi, Ally Salim apewe shavu la kukaa benchi kama kipa chaguo la pili maana anakuja vizuri kuliko Beno.

Awali lengo la uongozi wa Simba lilikuwa ni kuhakikisha wanakuwa na makipa bora wawili, ambao ni Beno na Aishi ndiyo sababu ya kumpiga chini Deo Munishi ‘Dida’. na kwenda kuvamia kwa mahasimu wao Yanga na kumng’oa Beno ambaye alikuwa na mzozo na kocha Mwinyi Zahera.

FILAMU ILIPOANZA

Habari zinasema kwamba waliporudi kambini baada ya corona, Beno aliambiwa na Mwarami kwamba ameongezeka uzito na anatakiwa kujifua zaidi.

Katika mechi za kikosi mazoezini kocha mkuu Sven Vandenbroeck aliwatumia Ally Salum na Aishi Manula huku Kakolanya akipewa filimbi achezeshe ili apate muda wa kukimbia uwanjani.

Katika mechi zile za kirafiki kwenye mchezo uliopigwa asubuhi dhidi ya Trans Camp Simba wakashinda mabao 4-2, Kakolanya alipewa dakika 45 za kipindi cha kwanza na kuruhusu goli moja kisha katika kipindi cha pili alicheza Ally Salim.

Kwenye mechi ya jioni yake dhidi ya KMC, Simba waliposhinda mabao 3-1, habari zinasema kipa aliyetakiwa kuanza ni Aishi na benchi kukaa Kakolanya lakini inadaiwa akaondolewa kutokana na Mwarami kutoridhishwa na mchezo wa asubuhi.

Habari zinasema kwamba hali hiyo iliendelea na kumfanya Kakolanya atupwe jukwaani dhidi ya Ruvu Shooting na Mwadui.

TIZI KIVYAKE

Baada ya kocha Vandenbroeck kuambiwa na Mwarami kwamba Beno hayupo fiti Jumatano iliyopita alimfanyisha mazoezi magumu ya kivyake asubuhi mpaka jioni huku akiwa na Mwarami tu.

KAKOLANYA AWEKWA KIKAO

Baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon jana kwenye Uwanja wa Uhuru asubuhi, Simba ikishinda mabao 5-0, Beno aliwekwa kikao.

Katika mechi hiyo kipa Ally Salim alisimama golini, huku Kakolanya akiachwa jukwaani ambapo gemu ilipomalizika Sven na Meneja, Patrick Rweyemamu walimuita Beno chini na kukaa faragha kwa dakika kadhaa kisha akapanda gari lake na kusepa.

Mwanaspoti lilimfuata kocha, Sven aweze kuzungumzia hali hiyo pamoja na kikao chao lakini akasisitiza; “Niko bize na kazi siwezi kuzungumza lolote.”

Mwarami naye alipotakiwa kufafanua kuhusiana na sakata hilo alisema kwa kifupi; “Mwenye mamlaka ya kuzungumza ni kocha mkuu.”

Lakini Beno mwenyewe alipoulizwa juu ya uwepo wa hali hiyo alionyesha kushangazwa na kinachoendelea dhidi yake kwamba yupo vizuri lakini hapewi muda wa kucheza.

“Niko vizuri lakini nashangaa kinachoendelea na sipewi muda wa kucheza kama awali,” alisema.

SOMA NA HII  LALA SALAMA INAHITAJI MAAMUZI MAKINI KWA SASA, MAMBO BADO HAYAJAWA SHWARI