Home Uncategorized MSHAHARA WA KOTEI YANGA KUFURU…!!

MSHAHARA WA KOTEI YANGA KUFURU…!!

KIUNGO James Kotei aliyesitishiwa mkataba na Slavia Mozyr ya nchini Belarus amefikia pazuri na Yanga ambao wamemuwekea Sh.80 milioni mezani asaini.

Mmoja wa vigogo wa Yanga alidokeza jana kwamba wanajua kuna watu wa Simba wanampigia Kotei wakimtaka awakaushie kwanza Yanga, lakini wao wana uhakika wa kumpata kwavile wanasubiria atue tu Ghana wakakae meza moja na wakala wake.

Kiongozi huyo alisema kwamba Yanga inataka kumpa Kotei kiasi cha dola 35000 (Sh 80.6 milioni) mkononi asaini ingawa meneja wake alikuwa anataka kiasi cha dola 40,000 (Sh92milioni) kwa mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo, mabosi wa Yanga wanaamini mara baada ya kiungo huyo kukutana nao uso kwa uso atalegeza na kuangukia wanapopataka ingawa ugumu unakuja kwamba Simba nao wananyemelea na alishafanya nao kazi awali anajua utamu wa mkwanja wao.

Habari zinasema kwamba wakala wa Kotei amewaambia Yanga kwamba anataka mteja wake acheze Jangwani kwavile pana njia nzuri ya kuchomoza kuliko Simba ambako kuna mastaa wengi.

Mbali na dau hilo la usajili Yanga pia inataka kumpa mshahara wa dola 3,500 (Sh 8 milioni) kwa mwezi huku awali mwenyewe alitaka alipwe dola 4,000(Sh 9.2 milioni).

Simba inafuatilia taarifa hizo za Kotei na Yanga na wanajua mpaka dau analotaka kupewa ambapo wamemwambia wanamfikiria akaushe kwanza ingawa na mchezaji huyo naye inadaiwa anahofia ushindani uliopo ndani ya Simba licha ya kwamba mara ya mwisho aling’ara vilivyo kabla hajauzwa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Simba na Yanga zimekuwa na tabia za kupigania wachezaji ambapo hilo kwa sasa limetokea pia kwa beki Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union, Michael Sarpong ambaye ni Mghana anayecheza Rayon Sports. Tayari Simba imemalizana na Sarpong ambaye ni straika.

Yanga tayari imeshamalizana na beki wa kushoto, Erick Rutanga wa kutoka Rwanda aliyekuwa akikipiga Police, vilevile winga Tuisila Kisinda wa AS Vita ya DR Congo.

Mbali na Kotei sasa Yanga inasaka saini ya washambuliaji Mpiana Mozizi ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Congo sambamba na straika mwenye nguvu raia wa Burkina Faso Sogne Yacouba ambaye wakala wake na Kotei ni mmoja.

SOMA NA HII  MPINZANI WA MWAKINYO ATIA TIMU BONGO KUTOKA ARGENTINA NA TAMBO KIBAO