JUNI 13, Yanga iliendelea pale ilipoishia kwa kutupa kete ya 28 mbele ya Mwadui FC mchezo uliochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na ya 29 mbele ya JKT Tanzania Juni 17.
Kocha Mkuu, Luc Eymael alipanga jeshi lote la kazi kwenye mechi hizo mbili ambazo ni dakika 180 nje ya Dar es Salaam ambapo aliambulia pointi nne pekee kati ya sita na kuziyeyusha pointi mbili.
Mfumo wake kwenye mechi zote hizo alizocheza alitumia 4-4-2 kusaka ushindi ndani ya uwanja.
Juni 17, Eymael aliongoza kikosi chake kupambana na JKT Tanzania kwenye mchezo huo Yanga ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1, ilikuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ukiachana na kadi nyekundu ambayo aliipata beki wa Yanga, raia wa Ghana, Lamine Moro kwa kucheza mchezo usio wa kiungwana kwa kiungo mstaarabu, Mwinyi Kazimoto kuna mengi ambayo raia huyo wa Ubelgiji anasema kuwa yalimpa ugumu kusepa na pointi zote sita.
Eymael amefunguka kuhusu mechi zake za mkoani ikiwa ni mara baada ya masuala ya michezo kuendelea baada ya kusimamishwa na Serikali kutokana na janga la Virusi vya Corona, Machi 17.
Eymael huyu hapa anaanza kufunguka namna hii:”Nimefurahi kurejea tena Tanzania kwani sikuwepo hapa kwa muda kidogo kutokana na kushughulikia masuala yangu ambayo yamekwenda sawa na nimerudi kamili.
Mechi mbili za nje ya Dar kwako zimekupa picha ipi?
“Nimeona namna ambavyo wachezaji wangu walikuwa wanajipanga wakati ule ligi iliposimama ila nina amini kwamba walifuata kile ambacho niliwaachia.
“Mechi mbili mfululizo tulikuwa nje ya Dar na mambo huko yalikuwa sio mazuri hasa kwa mazingira ambayo tulikuwa tupo nina amini ili kuongeza ubora zaidi wa ligi kuna mambo mengi yanahitaji maboresho.
Kipi kinahitaji maboresho?
“Kuanzia kwenye suala la miudombinu kuna masuala mengi ambayo hayapo vizuri, ukitazama kuanzia viwanja ambavyo tumetumia ni vibaya mfano wake hakuna na ni ngumu kupata matokeo mazuri.
Uwanja upi ulikupa shida?
“Utazame uwanja wa Kambarage ulivyo kisha achana na huo utazame Uwanja wa Jamhuri ni mbovu sijawahi kuona ninamaanisha kweli ni mbovu kabisa. Hivyo ilikuwa ngumu kwa wachezaji wangu kucheza ule mchezo ambao wameuzoea.
Aina ipi ya mchezo wa timu yako imezoea?
“Mpira wetu wa pasi na falsafa yetu ya kucheza kwa umakini. Nadhani uliona namna ambavyo tulicheza na Simba, Azam pale Uwanja wa Taifa zile ndo falsafa zetu sisi.
Kingine ni kipi ambacho kiliwapa tabu?
“Mazingira kiujumla yalikuwa mabaya,sehemu ya kubadilishia nguo za huko tulikokuwa si rafiki kiukweli inasikitisha kuona namna ambavyo wachezaji wanakuwa kwenye maandalizi katika mazingira magumu.
“Nina amini iwapo kutakuwa na maboresha mazuri katika miundombinu ni jambo jema ambalo litakuwa na manufaa kwa taifa kiujumla.
Pointi nne mlizovuna mlistahili?
“Tulistahili kubeba pointi zote sita kwani wachezaji walikuwa wanaonyesha ushindani nadhani kama ulifuatilia mechi kuna mabao ambayo tulifunga yalikataliwa. Licha ya mazingira kuwa magumu bado wachezaji walikuwa wanapambana.
Malengo makubwa kwa mechi ambazo mtatoka Dar yapoje?
“Ninajua bado tuna mechi nyingine ambazo tutatoka kwenda nje ya Dar ila tutajipanga ili kuona namna gani tunaweza kupata matokeo kwani kikubwa kwenye mchezo wowote ule tunahitaji pointi tatu,” anamaliza Eymael.
Mechi watakazopiga nje ya Dar ni dhidi ya Biashara United ya Mara, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Morogoro na Lipuli pale Iringa.Ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 31.