KOCHA Mkuu wa Namungo FC ya Lindi, raia wa Rwanda Hitimana Thierry, amefunguka kwamba kwa sasa anaiweka pembeni fainali ya Kombe la Shirikisho, maarufu kama FA, na mawazo yake anayapeleka kwenye mechi za Ligi Kuu Bara kwa ajili ya kufanikisha lengo lao la kumaliza katika nafasi ya nne.
Kocha huyo amesema kwa sasa akili zao hazitaiwaza fainali hiyo, badala yake wanaelekeza akili zao zote kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye ligi.
Namungo FC, walitinga fainali ya Shirikisho baada ya kuwafunga Sahare All Stars ya Tanga kwa bao 1-0 ambapo watamenyana na Simba.
Simba ilitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 4-1 mbele ya Yanga mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Julai 12.
Fainali ya FA inatarajiwa kuchezwa Agosti 2 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.
“Tunashukuru Mungu tumefika fainali ya Shirikisho ambapo kwa sasa tunahamisha mawazo yetu huku na tunarudi kwenye ligi.
“Tunataka kuangalia kwa namna gani tutamaliza kwenye nafasi ya nne tuliyopo kwenye ligi wakati huu tukiwa tunasubiri kucheza fainali ya kombe hilo,” alimaliza Hitimana.
Namungo wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wakiwa na pointi 60 baada ya kucheza mechi 34. Timu inayowafukuzia kwa karibu ni Coastal yenye pointi 51, iliyo katika nafasi ya tano