Home Uncategorized YANGA WANA JAMBO LAO, USAJILI WA MAJEMBE YA KAZI NI KAMILI ASILIMIA...

YANGA WANA JAMBO LAO, USAJILI WA MAJEMBE YA KAZI NI KAMILI ASILIMIA 90


KAMPUNI ya GSM kwa kushirikiana na Kamati ya Usajili ya Yanga tayari imekamilisha usajili wake kwa asilimia tisini katika kuelekea msimu ujao.

Yanga imepania kufanya usajili wa kisasa wenye ubora utakaoendana na hadhi ya timu yao ili kuhakikisha wanawapoka watani wao, Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara waliouchukua mara tatu mfululizo 2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020.
Mastaa wanaotajwa kuwepo kwenye rada za Yanga ni washambuliaji Tuisila Kisinda (AS Vita), Sogne Yacouba (huru), Heritier Makambo (Horoya AC), Jesse Were, Maric Makwata (Zesco), mabeki wa pembeni, Eric Rutanga (Rayon Sports), Yassin Moustapha (Polisi Tanzania).
Wengine ni Kibwana Shomari (Mtibwa Sugar),beki wa kati Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (La Galaxy), Ibrahim Ame ‘Varane’ (Coastal Union) na kiungo Ally Niyonzima (Rayon Sports).

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema kuwa asilimia 90 ya usajili wa wachezaji wa kimataifa kutoka nje ya nchi na wazawa umekamilika, hivyo watajiunga na kambi ya pamoja na wenzao haraka.

Bumbuli alisema kuwa wachezaji waliomalizana nao wote, ni wale waliotolewa mapendekezo na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Mbelgiji, Luc Eymael.
Aliongeza kuwa wametoa mapumziko ya wiki mbili kwa wachezaji na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi mara baada ya hapo haraka kikosi kitaingia kambini tayari kuanza msimu mpya wa ligi.

“Kwa asilimia 90 usajili wetu wa wachezaji wa kutoka nje ya nchi na wa ndani nikiwa na maana wazawa tayari umekamilika, tulianza kufanya mazungumzo nao muda mrefu wakati ligi inaendelea.
“Tulijitahidi kufanya kwa siri usajili huo kwa hofu ya wapinzani kuingilia kati, kwani mara kadhaa wamekuwa wakiingilia usajili wetu kwa kuwataka wachezaji tunaowahitaji na timu itaingia kambini baada ya wiki mbili kuanza maandalizi ya msimu mpya.

“Timu itaingia kambini tukiwa tumeshakamilisha usajili wetu kwa mujibu wa mapendekezo ya aliyekuwa kocha wetu Eymael ambaye aliikabidhi ripoti ya usajili katika michezo ya mwisho ya ligi.
“Tunategemea kuingia kambini katikati ya mwezi ujao kuelekea wiki ya Mwananchi mapema Septemba,” alisema Bumbuli.

Chanzo: Championi

SOMA NA HII  MARADONA HAYUPO FITI KIAFYA