IMERIPOTIWA kuwa nyota wa Klabu ya Barcelona, Lionel Messi amemwambia kocha wake mpya Ronald Koeman kwamba hana matumaini ya kuendelea kubaki ndani ya klabu hiyo kwa mujibu wa chombo kimoja cha radio RAC1.
Messi aliongea uso kwa uso na kocha mpya wa Klabu ya Barcelona Koeman ambaye amesaini dili la miaka miwili kuinoa klabu hiyo ambayo imetoka kupoteza kwa kichapo kikubwa cha mabao 8-2 mbele ya Bayern Munich ambayo itacheza mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG Agosti 23.
Ripoti zinaeleza kuwa Messi ameweka wazi kuwa hana imani na Rais wa Klabu ya Barcelona. Josep Bartomeu hivyo anatazama maisha yake ya baadaye.
Habari zinaeleza kuwa Messi anaweza kuibukia ndani ya Klabu ya Manchester City iliyo chini ya Kocha Mkuu, Pep Guardiola ambaye awali alikuwa anaamini kuwa Messi anapaswa kumalizia maisha yake ya mpira ndani ya Barcelona hivyo kwa sasa anaweza kuwashawishi mabosi wake wampe dili nyoa huyo mwenye miaka 33..
Koeman amesema kuwa itakuwa ngumu kumshawishi mchezaji ambaye anahitaji kuondoka ndani ya kikosi licha ya kwamba bado ni mali ya Barcelona.
“Bado ana mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Barcelona lakini sijui namna gani ninaweza kumshawishi abaki ndani ya timu,” amesema.