Home Uncategorized SIMBA YAFUATA KIUNGO URENO

SIMBA YAFUATA KIUNGO URENO


BAADA ya kukamilisha usajili wa Wabrazil wawili, mabosi wa Simba wamepanga kushusha kiungo kutoka nchini Ureno atakayekuja kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Wabrazil waliowasajili Simba ni kiraka, Gerson Fraga Vieira, anayemudu kucheza beki na kiungo mkabaji na mshambuliaji, Wilker Henrique da Silva wote waliosaini miaka miwili.

Simba, pia imefanikisha usajili wa kiungo mkabaji, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman anayekipiga klabu ya Al Hilal ya nchini Sudan.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, uongozi upo kwenye mazungumzo na kiungo huyo Mreno na kama mipango ikikamilika haraka atatua nchini kusaini mkataba.

Mtoa taarifa huyo alisema, tofauti na Mreno wataongeza wachezaji wengine watatu Wabrazil ambao wapo kwenye taratibu za mwisho kukamilisha mipango hiyo ya kumsajili.

“Mashabiki wa Simba watulie tena wawe watulivu kila kitu kitakwenda vizuri katika usajili wetu tupo kwenye taratibu za mwisho za kukamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

“Tayari tumefanikisha usajili wa wachezaji baadhi kati ya hao wawili kutoka Brazil na mwingine mmoja aliyetokea Sudan, pia tumepanga kusajili kiungo kutoka Ureno.

“Na kama mipango ikikamilika basi haraka tutamsajili kiungo Mreno mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi zote za kiungo namba 6 na 8, pia 10,’alisema mtoa taarifa huyo.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori hivi karibuni alisema kuwa “Mashabiki wa Simba waondoe hofu, uongozi umejipanga kukiimarisha kikosi chetu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na kikubwa tumejipanga kusajili mchezaji yeyote ndani nje ya Afrika.”

SOMA NA HII  ACHENI KULALAMIKA, UNACHOPATA SASA NI KILE ULICHOPANDA 2018/19