LIGI Kuu Bara inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 6, huku msimu huu tukizishuhudia jumla ya timu 18 zikipambana kuwania ubingwa ambao unashikiliwa na Simba kwa msimu wa tatu mfululizo. Timu za Dodoma FC, Gwambina na Ihefu zikionja kwa mara ya kwanza ladha ya Ligi Kuu Bara baada ya kupanda daraja.
Hizi hapa baadhi ya pacha ambazo zinapewa nafasi ya kutikisa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na usajili ambao unaendelea kufanyika hadi sasa…
CLATOUS CHAMA, LUIS MIQUISSONE NA BERNARD MORRISON-SIMBA
Ni moja ya pacha ambazo zinasubiriwa kwa hamu kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na uwezo mkubwa wa wachezaji hao. Hii inatarajiwa kuwa moja ya pacha tishio kwenye safu ya kiungo cha ushambuliaji ndani ya timu hiyo, Morrison anaungana na Miqussone na Chama baada ya kukamilisha dili lake la kujiunga na Simba kwa miaka miwili akitokea Yanga SC.
BAKARI MWAMNYETO NA LAMINE MORO-YANGA
Msimu uliopita, safu ya ulinzi ya Yanga iliruhusu jumla ya mabao 28 kwenye mechi 38, hivyo basi usajili wa Mwamnyeto kutoka Coastal Union unatarajiwa kutengeneza safu imara ya ulinzi kwa kushirikiana na beki kisiki wa timu hiyo, Lamine Moro.
VITALIS MAYANGA NA YUSUPH MHILU-KAGERA
Kagera Sugar imefanikiwa kumbakisha kikosini nyota wake Yusuph Mhilu huku wakimuongeza kikosini mshambuliaji wa zamani wa Ndanda, Vitalis Mayanga.
Mhilu ameifungia Kagera Sugar jumla ya mabao 13 kwenye Ligi Kuu Bara huku Mayanga akimaliza msimu na mabao saba kwenye ligi hiyo, uwezo wa nyota hawa unatarajiwa kutengeneza moja ya pacha hatari zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
AWESU AWESU, ABUBAKAR SALUM NA ALLY NIYONZIMA –AZAM
Azam FC pia ni miongoni mwa timu ambazo zimefanya usajili wa uhakika msimu huu kwa kuwaongeza kikosini nyota kadhaa akiwemo Mnyarwanda Ally Niyonzima na kiungo Awesu Awesu aliyejiunga na timu hiyo akitokea Kagera Sugar.
Viungo hawa wanatarajiwa kutengeneza pacha bora kwenye kikosi chao ukizingatia wote ni wachezaji wenye uwezo mkubwa, Sure Boy amekuwepo ndani ya kikosi cha Azam kwa miaka takriban 12, hivyo basi kuongezeka kwa Awesu na Niyonzima kutaongeza ubunifu kwenye safu ya kiungo ya timu hiyo na kuifanya kuwa moja ya pacha hatari na za kuchungwa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
LUCAS KIKOTI, ABDULHALIM HUMUD NA SIXTUS SABILO-NAMUNGO
Sabilo alikuwa kwenye kiwango bora akikipiga kwenye kikosi cha Polisi Tanzania akitengeneza pacha matata na Marcel Kaheza, kuwepo kwake ndani ya Namungo akishirikiana na Adulhalim Humud na Lucas Kikoti inatarajiwa kuwa moja ya pacha hatari zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao.
IBRAHIM AME NA JOASH ONYANGO-SIMBA
Ingizo jipya ndani ya Simba, Ame na Onyango ni moja ya mabeki wenye uwezo mkubwa na wanatarajiwa kutoa upinzani mkali kwa wakongwe Paschal Wawa na Erasto Nyoni ndani ya Simba, Onyango amejiunga na Simba akitokea Gor Mahia ambapo alifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Kenya msimu wa 2018/19.
Ame amejiunga na Simba akitokea Coastal Union alipokipiga kwa mafanikio makubwa msimu uliopita, endapo watafanikiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza ndani ya Simba inatarajiwa kuwa moja ya pacha kali zaidi Ligi Kuu Bara msimu ujao.
JACOB MASSAWE NA PAUL NONGA-GWAMBINA
Gwambina FC imefanikiwa kuinasa saini ya nahodha wa zamani wa Lipuli FC Paul Nonga kwa kandarasi ya mwaka mmoja , huku Massawe akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza.
Nonga na Massawe wanatarajiwa kutengeneza pacha kali ya utupiaji mabao ndani ya kikosi hicho kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao kutokana na nyota hao kuwa na uwezo mkubwa wa kutupia mabao.
ZAWADI MAUYA, FEISAL SALUM NA HARUNA NIYONZIMA-YANGA
Safu ya kiungo ya Yanga msimu ujao inatarajiwa kutawaliwa na viungo wanyumbufu na wenye uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu.
Ongezeko la Mauya ndani ya kikosi cha Yanga linatarajiwa kuongea ubunifu kutokana na uwezo wa kiungo huyo, uwepo wa Niyonzima na Fei Toto kwa kiasi kikubwa unatarajiwa kutengeneza pacha matata kwenye eneo la kiungo la timu hiyo kwa msimu ujao.