BERNARD Morrison, winga mpya wa Klabu ya Simba rasmi atakipiga kwenye klabu hiyo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania kumtambulisha kwamba ni mchezaji wa timu hiyo.
Agosti 30 kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi Yanga ilimtambuisha Morrison kuwa mmoja kati ya wachezaji wake 28 kwa kueleza kuwa mchezaji huyo kesi yake ipo Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Masuala ya Wachezaji,(Cas).
Mchezaji huyo pia Agosti 22 kilele cha Simba Day alitambulishwa kuwa mchezaji wa Simba na Agosti 30 jambo lililomfanya awe mchezaji pekee aliyetambulisha mara mbili ndani ya Uwanja Mkapa.
Morrison aliyekuwa na mvutano na mabosi wake hao wa zamani, alitajwa kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi kama mchezaji wa Yanga, akiwa jijini Arusha kukinukisha kwenye mechi ya Ngao ya Jamii ya timu yake mpya ya Simba iliyoishinda Namungo kwa mabao 2-0.
Lakini mashabiki wakiwa bado hawaamini kama nyota huyo aliyewapa raha msimu uiliopita kwa kuwatungua Simba katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara, atasalia kikosini mwao, katika orodha ya usajili mpya ya TFF kwa msimu ujao jina lake limetokezea Simba kuonyesha ni mali yao rasmi sasa.
Ofisa habari wa TFF, Cliford Ndimbo, amesema kilichomfanya Morrison awe kwenye orodha ya Simba badala ya ile ya Yanga ni kwa kuzingatia maamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji iliyomtambulisha kama mchezaji huru baada ya kusikiliza kesi iliyomhusisha Mghana huyo na Yanga.