NAHODHA wa sasa wa Yanga, Deus Kaseke, amefunguka kwamba, amejipanga kuendana na uwepo wa wachezaji wengi wapya ndani ya klabu hiyo, ili asije akateleza na kukosa namba.
Benchi la ufundi la Yanga limeamua kumpa Kaseke kitambaa cha unahodha baada ya manahodha wa msimu uliopita, Papy Kabamba Tshishimbi na Juma Abdul kutemwa.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kaseke ameweka wazi kuwa, kufuatia kuwepo na maboresho makubwa ndani ya kikosi hicho, naye ameongeza uwezo wa kupambana kwenye kikosi ili kuendana na wimbi la kutokosa namba.
“Siku zote unapokuwa katika kikosi chenye uwezo mkubwa ni vyema kuhakikisha na wewe unaongeza juhudi ili usikose namba kikosini.
“Kwa sasa natumika nikiwa nahodha wa timu, hivyo ni jukumu langu kujituma ili niwape hamasa zaidi wenzangu.
“Haipendezi nahodha kama mimi niwe nakosa namba katika kila mechi, maana nikiruhusu hilo nitakuwa siwapi hamasa wenzangu ya kupambana, raha ya kuwa nahodha upate muda wa kucheza na siyo kukaa benchi,” alisema Kaseke.
Yanga itaanza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa kumenyana na Tanzania Prisons mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa majira ya saa 1:00 usiku. Itakuwa ni Septemba 6.