NYOTA wa Klabu ya Barcelona, Lionel Messi amesema kuwa sababu kubwa ya kubaki ndani ya klabu hiyo ni kutotaka kwenda mahakamani kwa ajili ya shauri lake la kutaka kuvunja mkataba kwa kuwa anaipenda timu hiyo.
Messi alikuwa anahitaji kuondoka ndani ya kikosi hicho na timu ambayo ilikuwa inapewa nafasi kuipata saini yake ilikuwa ni Manchester City inayoshiriki Ligi Kuu England.
Nyota huyo mwenye miaka 33 amethibitisha kuwa atabaki ndani ya Barcelona kwa msimu ujao kwa sababu timu hiyo iliweka vizuizi katika masuala yake ya kutaka kuondoka ndani ya timu hiyo jambo ambalo limemfanya asitake kuingia kwenye mgogoro na mabosi zake hao.
Messi amesema Barcelona ilikuwa inahitaji alipe kiasi cha pauni milioni 625 jambo ambalo ni gumu kwake kuweza kulifanya na haliwezekani kukamilika kwa wakati wa sasa.
“Nitaendelea kubaki ndani ya timu hii kwa sababu nimeambiwa kwamba kama ninahitaji kuondoka basi ninapaswa kulipa pauni milioni 625 haiwezekani kutokea hili jambo.
“Sitaki kuingia kwenye mgogoro na timu yangu kwa sasa kwa kuwa ninaipenda hivyo nitabaki hapa na nitacheza pia,” amesema.
Baada ya Barcelona kuchapwa mabao 8-2 mbele ya Bayern Munich kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Messi alikuwa kwenye hesabu za kutaka kuondoka ndani ya timu hiyo na alimwambia Kocha Mkuu, Ronald Koeman kuwa anataka kuondoka lakini kwa sasa atabaki ndani ya kikosi hicho.