BAADA ya Prince Dube kuifungia Azam FC bao la ushindi dhidi ya Tanzania Prisons ni wazi nyota huyo anakula sahani moja na washambuliaji kama Meddie Kagere na Chris Mugalu, ambao wamekuwa na uwiano mzuri wa kufunga.
Dube tangia asajiliwe na Azam amekuwa na kiwango kizuri hususani katika michezo ya ligi kuu mara baada ya kufanikiwa kufunga mabao matatu na kutoa pasi ya bao moja katika michezo minne aliyoichezea timu hiyo.
Dube katika michezo hiyo minne aliyoichezea Azam alifanikiwa kufunga katika michezo miwili dhidi ya Coastal Union alipofunga mabao mawili kisha akafunga bao moja katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.
Michezo mingine ni dhidi ya Polisi Tanzania ambapo alitoa pasi ya bao lililofungwa na Obrey Chirwa huku katika mchezo dhidi Mbeya akishindwa kufunga wala kutoa pasi ya bao.
Baada ya kufunga mabao hayo matatu kwenye ligi, Dube ni wazi anakula sahani moja na washambuliaji wengine kama Meddie Kagere na Chris Mugalu wa Simba ambao wamefunga mabao mawili kila mmoja.
Kwa sasa Azam FC inaongoza ligi ikiwa imeshinda mechi zake zote nne na imefunga mabao matano na haijaruhusu bao la kufungwa katika mechi hizo.
Matokeo yake yapo namna hii: Azam FC 1-0 Polisi Tanzania, Azam FC 2-0 Coastal Union ilikuwa Uwanja wa Azam Complex, Mbeya City 0-1 Azam FC Uwanja wa Sokoine na Tanzania Prisons 0-1 Azam FC Uwanja wa Nelson Mandela.