Home Uncategorized KIPCHONGE MAMBO MAGUMU ASHINDWA KUTETEA TAJI LAKE KISA MAUMIVU YA NYONGA

KIPCHONGE MAMBO MAGUMU ASHINDWA KUTETEA TAJI LAKE KISA MAUMIVU YA NYONGA


 Eliud Kipchoge, bingwa wa mbio za marathon ameshindwa kutetea taji lake la London marathon Jumapili baada ya kuishiwa nguvu katika kilomita 35 za mbio hizo na kujikuta akimaliza katika nafasi ya nane.

 

Shura Kitata wa Ethiopia alitwaa ushindi kwa kumponyoka Mkenya Vincent Kipchumba katika sekunde za mwisho kabisa na kumaliza mbio hizo katika muda wa saa 2, dakika 5 na sekunde 41. 


Kepchumba alimaliza wa pili sekunde moja baadaye na nafasi ya tatu ilichukuliwa na mkimbiaji mwingine kutoka Ethiopia, Sisay Lemma, katika muda wa saa 2, dakika 5 na sekunde 45.

 

Akizungumza baada ya mashindano hayo, Kipchoge alisema, “Nimesikitika sana. Nilikuwa na tatizo na sikio langu la kulia baada ya kuziba na kisha nikawa na maumivu ya tumbo na matatizo ya nyonga. Kulikuwa na baridi lakini silaumu mazingira hayo.”

 

Mbio za London marathon zilielekea kuwa kali mwaka huu zikiwapambanisha Eliud Kipchoge na Kenenisa Bekele wa Ethiopia ambao walidhaniwa kuwa na nafasi kubwa sana ya kushinda katika mbio hizo. Lakini hali ilianza kubadilika siku mbili kabla ya mbio pale Bekele alipotangaza kujitoa katika mbio hizo kutokana na maumivu aliyokuwa nayo.

 

Kujitoa kwa Bekele kuliuacha uwanja wazi kwa Kipchoge na ilielekea hivyo kwa sehemu kubwa ya mbio hizo ambazo mwaka huu hazikutumia njia ya kawaida badala yake ilikuwa mizunguko ya eneo maalum lililotengwa.

 

Lakini hali ilianza kubadilika katika kilomita ya 35 pale Kipchoge alipoanza kupunguza kasi na kundi la akina Kitata, Kepchumba, Lemma na wengine wakachukua fursa hiyo kumtoka haraka bingwa huyo wa dunia.

SOMA NA HII  STARS YAPATA MAKOCHA WAWILI WAPYA, WAANZA KAZI MOJAKWAMOJA