ZAKARIA Thabit, Ofisa Habari wa Azam FC amesema kuwa malengo makubwa yaliyopo kwenye timu hiyo ni kuweza kubeba moja ya taji katika mashindano makubwa watakayoshiriki kwa msimu huu wa 2020/21.
Azam FC ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tano za ligi.
Imeshinda mechi zote ikiwa imefunga jumla ya mabao tisa na kufungwa mabao mawili ndani ya dakika 450.
Akizungumza na Saleh Jembe, Zakazi amesema kuwa mpango mkubwa ni kuona kwamba wanaweza kurejesha makali ambayo waliyakosa msimu uliopita.
“Tupo kwenye wakati wa mapambano kwa sasa na kila mchezaji pamoja na mashabiki nadhani wanaona namna ambavyo tunafanya.
“Kikubwa kwa msimu huu ni kuona kwamba kwenye mechi zetu za mwanzo hizi ambazo tumeanza vizuri iwe na mwendelezo mzuri wakati wote.
“Mashabiki wetu na wadau wa Azam FC waendelee kuwa pamoja nasi kwani tuna jambo letu,” amesema.
Azam FC inashiriki kwenye mashindano makubwa mawili ambayo ni Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho na yote yapo mikononi mwa Simba.