MSHAMBUALIAJI wa zamani wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe amefunguka kuwa Yanga imepata bonge la Kocha Cedric Kaze ambaye anapenda soka la pasi za chini huku akiwatahadharisha wapinzani wao wajipange kwa soka tamu la pasi.
Tambwe ametoa kauli hiyo baada ya uongozi wa Yanga kumalizana na Kaze ambaye anakuja kubeba mikoba ya Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyesitishiwa kibarua chake.
Tambwe aliyewahi kuichezea Yanga alisema kwa Kaze, Yanga wamepata kocha mzuri anayependa kufundisha soka la pasi hivyo wapinzani wao wajipange vizuri kuona moto wake.
“Kaze ni kocha mzuri kutokana na jinsi ninavyomjua tangu zamani wakati nacheza Vital’O hapa Bujumbura, yeye alikuwa akifundisha Atletico, kweli timu yake ilikuwa inacheza mpira wa chini wenye pasi nyingi.
“Nadhani labda kitu ambacho kinaweza kusumbua ni hizo presha za Tanzania labda huenda ndiyo zikawa tatizo kwake, unajua tangu ameondoka Bunjumbura kwenda Ulaya amekuwa akifanya kazi na timu za watoto, mtu akizoea timu za watoto inakuwa tofauti.
“Lakini nje ya hapo Kaze ni kocha mzuri, anafundisha mpira wa chini siyo wa kutupa tupa yaani ule wa kubutua butua naamini atawasaidia sana Yanga kwa kuifanya icheze mpira mzuri, wapinzani wanatakiwa kujiweka sawa kweli.
“Kikubwa ambacho kinaweza kumsumbua hapo Tanzania labda presha za mashabiki zinaweza kumsumbua, nafikiri wampe muda kwanza ataijenga vyema timu na itacheza soka la pasi nyingi za chini.” amesema.
Kaze anatarajiwa kutua nchini Alhamisi kuanza kukinoa kikosi cha Yanga ambacho kwa sasa kipo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi.
Chanzo: Championi