HITIMANA Thiery, Kocha Mkuu wa timu ya Namungo amesema kuwa kwa sasa ni upepo mbaya unawasumbua ndani ya uwanja jambo ambalo linawafanya washindwe kupata matokeo chanya.
Msimu wa 2019/20 ilipoteza mchezo mmoja pekee Uwanja wa Majaliwa ilikuwa ni dhidi ya Coastal Union ila kwa msimu huu wa 2020/21 tayari imeshapoteza mechi mbili ikiwa nyumbani.
Ilianza kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania na ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC jambo ambalo limetibua rekodi yakeya msimu wa 2019/20.
Thiery amesema kuwa upepo umekuwa ni mbaya kwa msimu huu wa 2020/21 jambo linalofanya timu yake inapoteza.
“Huwezi kuwa na matokeo mazuri muda wote hasa kwenye maisha ya ligi, kwa sasa naona upepo umekuwa mbaya kwetu kwa kuwa tunapata matokeo ambayo hatuyafurahii, bado tunajiweka sawa ili kushinda mechi zetu zijazo.
“Ninajua kwamba kila mmoja anahitaji matokeo mazuri hata mimi pia ninapenda kuona hivyo, ila kwa namna ushindani ulivyo kuna wakati mwingine unapaswa ukubali kwamba mambo siyo mazuri kwako, ” amesema.
Mchezo ujao kwa Namungo itakuwa ni Oktoba 14 itacheza na Kagera Sugar Uwanja wa Majaliwa.
Namungo ipo nafasi ya 9 imecheza mechi tano inakutana kesho na Kagera Sugar iliyo nafasi ya 13 na pointi zake nne.