KIUNGO wa Simba, Clatous Chama ana matumaini makubwa ya timu yao kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Novemba 20, mwaka huu ambapo michezo ya hatua ya awali itapigwa.Kwa msimu wa 2020/21, Simba ndiyo wawakilishi pekee wa michuano hiyo.
Akizungumzia nafasi ya Simba kwenye michuano hiyo, Chama alisema: “Nawapongeza viongozi kwa kufanya usajili bora, ukiachana na mashindano mengine tutakayoshiriki, tunafahamu tuna kibarua cha Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Zimebaki siku chache kabla ya kuanza michuano hiyo, naona kila mchezaji hapa anajitahidi kuboresha kiwango chake ili kuingia kwenye kikosi cha kwanza.
Naamini ubora wa kikosi cha msimu huu na funzo la kuaga mashindano mapema msimu uliopita ni vitu vitakavyotufanya tufanye vizuri.”
Simba ilitwaa ubingwa msimu wa 2019/20 jambo linalowapa nafasi ya kushiriki michuano mikubwa Afrika ya Ligi ya Mabingwa inayowahusisha mabingwa wa ligi za timu za Afrika.
Kwa sasa ipo zake Mbeya ambapo imekwenda kwa ajili ya kuweka kambi kwa muda wa siku mbili kabla ya kuelekea Rukwa kuwafuata wapinzani wao Tanzania Prisons.
Mchezo huo wa ligi utachezwa Oktoba 22, Uwanja wa Nelson Mandela.