CEDRIC Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kikubwa ambacho anakihitaji kuona kutoka kwa wachezaji wake ni kupata ushindi utakaowafanya wasepe na pointi tatu muhimu ndani ya uwanja.
Mechi ya kwanza Kaze alikiongoza kikosi chake Oktoba 22 mbele ya Polisi Tanzania na alishinda bao 1-0 Uwanja wa Uhuru.
Kwa sasa kikosi cha Yanga kitakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC utakaochezwa Oktoba 25 Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza ambapo kimeshatia timu Mwanza leo.
Kaze amesema kuwa anaona wachezaji wake wanapambana ndani ya uwanja kwenye kusaka matokeo jambo linalompa faraja.
“Kikubwa ambacho ninahitaji kutoka kwa wachezaji ni kuona kwamba timu inapata ushindi na kupata pointi tatu haijalishi ni idadi ipi ya mabao.
“Kwa namna ambavyo tumeanza sio mbaya kwani bado kuna makosa yapo ambayo ni muhimu tuyafanyie kazi, bado mambo yanakuja ila kwa sasa acha tuanze na pointi tatu,” amesema.
Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi sita imeshinda mechi tano na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Tanzania Prisons Uwanja wa Mkapa.