KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji, ameonekana kuteseka kwa dakika 270 ambazo ni sawa na mechi tatu mbele ya kocha mzawa, Charles Boniface Mkwasa.
Sven na Mkwasa wamekutana mara nne katika michuano yote na Mkwasa kuonekana kufanya vizuri katika mechi tatu ambapo ameshinda mbili na sare moja, huku akipoteza moja mbele ya Mbelgiji huyo.
Mkwasa ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa kikosi cha Ruvu Shooting, alianza kukutana na Sven Januari 4, mwaka huu katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika kwa sare ya 2-2.
Katika mchezo huo, Mkwasa ndiye aliyekuwa kocha anayekinoa kikosi cha Yanga ambapo alipindua meza kibabe kutoka 2-0 hadi 2-2 dhidi ya Simba.
Machi 8, mwaka huu, Mkwasa akiwa kocha msaidizi wa Yanga, timu yake ilishinda 1-0 dhidi ya Simba ya Sven katika Ligi Kuu Bara.
Julai 12, mwaka huu, Simba ya Sven iliichapa Yanga mabao 4-1 katika nusu fainali ya Kombe la FA. Hapa Mkwasa alikuwa kocha msaidizi wa Yanga.
Oktoba 26, ilishuhudiwa Mkwasa akiliongoza jeshi la Ruvu Shooting, alishinda 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar.
Mechi tatu za kwanza, wawili hao walipambana Uwanja wa Mkapa jijini Dar na Sven alioja joto ya jiwe.