CEDRIC Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United.
Mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 31, utakuwa ni wa tatu kwa Kaze kukaa kwenye benchi baada ya kusaini dili la miaka miwili.
Tayari amekaa benchi kwenye mechi mbili na kushuhudia wachezaji wake wakifunga mabao matatu na kufungwa bao moja huku wakikusanya jumla ya pointi sita.
Alianza mbele ya Polisi Tanzania wakati Yanga ikishinda bao 1-0 Uwanja wa Uhuru na alishinda mabao 2-1 dhidi ya KMC, Uwanja wa CCM Kirumba.
Wachezaji wake wanatarajiwa kuingia uwanjani Oktoba 31, Uwanja wa Karume kumenyana na Biashara United inayonolewa na Francis Baraza.
Kaze amesema:”Mechi yetu dhidi ya Biashara United itakuwa na ushindani mkubwa ila ninaona kwamba bado tuna nafasi ya kushinda mchezo huo kwa kuwa wachezaji wanaonyesha ari na morali kubwa.
“Kikubwa ninawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu yao,” amesema.
Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ina pointi 19 ikiwa imecheza mechi saba za ligi. Msimu uliopita ilipokutana na Biashara United Uwanja wa Karume ililazimisha sare ya bila kufungana.