SALUM Abubakar, kiungo wa Azam FC maarufu kama Sure Boy amesema kuwa ana imani kwamba kikosi hicho kitafikia malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na kasi ambayo wameanza nayo.
Azam FC ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa wamecheza mechi tisa na kujiwekea kibindoni jumla ya pointi 22 na safu yao ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 15.
Kwenye mabao hayo, Sure Boy amehusika jumla kwenye mabao mawili ambapo amefunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao.
Mchezo wa kwanza kwa Azam FC ilikuwa ni mbele ya Mtibwa Sugar ilifungwa bao 1-0 baada ya kucheza mechi saba bila kupoteza na ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni sare yao ya kwanza kwa msimu wa 2020/21.
Sure Boy amesema::”Mipango ipo sawa na kila mchezaji anatambua kwamba ushindani ni mkubwa, imani yangu ni kuona kwamba kikosi kinaweza kutimiza malengo ambayo imejiwekea ikiwa ni pamoja kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2020/21.”
Mabingwa watetezi wa ligi ambao ni Simba wao wamejichimbia nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi nane ndani ya ligi na pointi zake ni 16.