KOCHA Mkuu wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze, amefunguka kuwa licha ya mwenendo usio mzuri walionao wapinzani wao Gwambina FC lakini bado wataingia uwanjani leo Jumanne wakiwa wanawaheshimu.
Kaze ameongeza kuwa kinachowafanya waingie wakiwa wanawaheshimu wapinzani wao ni kuwa wapo nyumbani kwao lakini mawazo yake ni kupata pointi tatu mbele yao.
Kaze kwa mara nyingine leo Jumanne ataiongoza Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara kupambana na Gwambina FC katika muendelezo wa mechi zao za Kanda ya Ziwa.
Mrundi huyo amesema kuwa licha ya nia yao ya kutwaa pointi tatu lakini watakuwa makini kwa sababu wapinzani wao wana safu nzuri ya ushambuliaji na pia wanacheza uwanjani kwao.
“Kuhusiana na Gwambina wao wako nyumbani na wamefanya vizuri kwenye eneo lao la ushambuliaji. Hatuwezi kuwadharau kwa sababu walifungwa mechi iliyopita kwa mabao 3-0 na KMC.
“Tunaingia kwa nguvu kubwa kwenye mechi hiyo tukiwa na nia ya kutaka kupata pointi tatu kama ambavyo tumefanya kwenye mechi zilizopita,” alimaliza Kaze.
Mchezo huo utachezwa leo Novemba 3, Uwanja wa Gwambina Complex. Yanga mechi yao iliyopita ilishinda bao 1-0 dhidi ya Biashara United ya Mara.
Bao la ushindi kwa Yanga lilifungwa na Michael Sarpong ambaye ana jumla ya mabao mawili ndani ya ligi.