Home Uncategorized BOSI SIMBA AOMBA VAR KWENYE DABI

BOSI SIMBA AOMBA VAR KWENYE DABI

 


ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo, amesema inahitajika VAR (Video Assistant Referee) kwa ajili ya kung’amua matukio tata ikiwemo penalti ambayo walipata wapinzani wao Yanga walipocheza nao Novemba 7.

 

Hans Poppe ameongeza kwamba VAR hiyo itakuwa msaada mkubwa wa kutoa haki baada ya waamuzi wengi kuonekana kuwa na upungufu kwenye maamuzi hasa kwenye dabi kati ya Simba na Yanga. Bosi huyo amesema hayo baada ya Simba kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Kwenye mechi hiyo, Yanga ilipata penalti iliyozua utata dakika ya 28 iliyosababishwa na Tuisila Kisinda aliyeangushwa na beki Joash Onyango. Dabi hiyo ilisimamiwa na waamuzi sita ambao waliongozwa na Abdallah Mwinyimkuu.

 

Baada ya mechi hiyo, Hans Poppe alisema kwa sasa inahitaji VAR ambayo itatoa majibu ya ukweli ya matukio ya namna hiyo baada ya waamuzi wengi kushindwa kwenda sawa na kasi ya mechi hiyo.

 

“Mchezo umeisha na imekuwa droo, lakini mimi napiga kelele na uchezeshaji wa marefa wetu. Waliona penalti moja upande wetu ambayo hata pengine siyo lakini penalti zetu tatu ambazo ziko wazi hawakuziona.

 

“Tunafanyiwa fujo lakini mwamuzi hatoi kadi yoyote ile sijui wanashindwa kumudu kwa sababu ya woga, kiukweli uchezeshaji kiujumla haukunifurahisha. Kwa namna hii haki haitendeki na anayestahili kushinda hashindi.

 

“Hata waweke waamuzi 20 lakini kwa namna hii wakiendelea kufanya makosa nafikiri tulete VAR itatutatulia mambo yote,” aliweka nukta Hans Poppe.

SOMA NA HII  FA KUFUNGUA DIRISHA LA USAJILI AGOSTI